Mshukiwa wa dawa za kulevya arudishwa Kenya

Raia wa Kenya, Ndechumia Bilali Kimali anayedaiwa kuwa mlanguzi wa madawa ya kulevya alirejeshwa humu nchini Jumatatu asubuhi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani. Haki miliki ya picha AFP
Image caption Raia wa Kenya, Ndechumia Bilali Kimali anayedaiwa kuwa mlanguzi wa madawa ya kulevya alirejeshwa humu nchini Jumatatu asubuhi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani.

Mkenya, anayeshukiwa katika ulanguzi wa madawa za kulevya afukuzwa Madagascar

Raia wa Kenya, Ndechumia Bilali Kimali anayedaiwa kuwa mlanguzi wa madawa ya kulevya alirejeshwa humu nchini Jumatatu asubuhi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani.

Kimali alitorokea Madagascar Aprili mwaka wa 2015 baada ya kuhusishwa na dawa za kulevya aina ya heroine yenye kilo 7.6 iliyopatikana kwenye meli ya MV Baby Iris. Meli hiyo baadae ililipuliwa na maafisa usalama wa Kenya kwenye bahari hindi.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, mkuu wa Idara ya Ujasusi katika Mamlaka ya viwanja vya ndege, KAA, Joseph Mugwanja amesema jamaa huyu huenda akawa ni mmoja wa watu wanaoendesha biashara hii humu nchini na pia nje ya nchi.

''Kila mtu anafaa kufahamu kuwa magaidi wote wanaofanya uhalifu humu nchini na kutorokea nchi nyingine watafuatwa na kurejeshwa humu na kuadhibiwa kulingana na sheria." Mugwanja alisema.

Kimali alisindikizwa na afisa wawili wa polisi wa Madagascar ambao walimkabidhi kwa polisi wa Kenya .

''Maafiasa wetu wa usalama wanashirikiana na wengine nje ya nchi kuhakikisha wahalifu hawapati nafasi ya kutenda maovu kwingineko."

Meli ya MV Baby Iris ilikuwa imebeba madawa ya heroine yenye thamani ya dola 228,000 na operesheni ya kuilipua iliongozwa na Waziri wa Usalama Joseph Nkaiserry.

Washukiwa wengine ambao tayari wamefikishwa mahakamani ni raia wa Ushelisheli aliyekuwa nahodha wa meli hiyo, Clement Serge Bristol na Wakenya Ahmed Said, Mohamed Bakari Mohamed, Sharifu Mzee Mohamed na Ahmed Hussein Salim.

Hii ilikuwa ni mara ya pili kwa serikali ya Kenya kulipua meli iliyobeba mihadarati.

Mnamo Agosti, 2014, rais Uhuru Kenyatta alishuhudia mafisa wa usalama wakitumia vilipuzi kwenye meli iliyobeba heroine yenye thamani ya dola milioni 10.

Meli iliyobeba madawa hayo ya kulevya ilinaswa kisiwani Lamu.