Uchaguzi Kenya: Ni kwa nini Odinga hataki kwenda kortini?

Haki miliki ya picha Getty Images

Hata kabla ya matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais nchini Kenya kutangazwa Ijumaa tarehe 11 Agosti, muungano wa upinzani nchini humo ulikuwa umechukua msimamo usiokuwa wa kawaida - kwamba hautawasilisha kesi mahakamani kupinga matokeo hayo licha ya kutoyakubali.

Hilo lilishangaza kwani katika mataifa ya kidemokrasia, mahakama huwa ndiyo taasisi iliyo na jukumu la kuhakikisha haki inatendeka iwapo raia au taasisi yoyote itajihisi kutotendewa haki.

Aidha, ndiyo njia pekee iliyosalia sasa ambayo inaweza kumpa tena Bw Raila Odinga matumaini ya kuingia madarakani au kujaribu tena kuingia madarakani iwapo itabatilisha ushindi wa Bw Kenyatta.

Muungano huo ulikuwa siku moja baada ya uchaguzi kufanyika, umeandaa kikao na habari na kutangaza kwamba walikuwa wamegundua mitambo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) ilidukuliwa.

Walidai wadukuzi walikuwa watu wenye uhusiano na serikali ya Jubilee na kwamba waliingilia na kuchakachua matokeo kumfaa Rais Uhuru Kenyatta aliyekuwa akishindana na Bw Raila Odinga kwa mara ya pili.

Kuhusu tuhuma hizo za udukuzi, walipotakiwa kutoa maelezo zaidi kuhusu ni nani hasa aliyehusika, pamoja na jinsi walivyopata nyaraka za taarifa kuhusu sava matukio katika sava moja ya tume hiyo, walikataa kata kata.

Samahani, kisakuzi chako hakiwezi kuonesha ramani hii

Tume ya uchaguzi ilisema mwanzoni ilikuwa haina taarifa kuhusu udukuzi kama huo lakini kwamba ingelifanya uchunguzi. Saa chache baadaye, tume hiyo ilisema hakuna jaribio lolote la udukuzi lililokuwa limefanyia katika sava ya matokeo ya uchaguzi.

Waliofuatilia kisa hiki, walitarajia kwamba huu ungekuwa msingi wa muungano wa upinzani National Super Alliance katika kupinga matokeo ya urais kortini.

La pili lilikuwa tuhuma kuhusu sajili ya wapiga kura, ambapo kabla ya uchaguzi kufanyika, muungano huo ulikuwa umedai tume ilikiuka sheria katika kuchapisha orodha rasmi ya wapiga kura vituoni ndipo wananchi waihakiki na kuhakikisha kuna uwazi.

Baadhi ya wanachama wa NASA walidai kuna watu waliokuwa wamefariki ambao walikuwa bado kwenye sajili hiyo, na wengine ambao hawakuwa wametimiza umri wa kupiga kura ambao walikuwa na vitambulisho na walikuwa kwenye sajili. Tume ya uchaguzi ilikanusha tuhuma zote.

Naibu ajenti mkuu wa Nasa, seneta James Orengo alisema saa chache kabla ya matokeo kutangazwa: "Kwenda kortini si njia ambayo tutatumia, tumekuwa huko awali. Si njia ambayo tutatumia… Kila wakati uchaguzi ukiibiwa, Wakenya wamesimama na kuhakikisha mabadiliko yanafanyika kuimarisha nchi."

"Hakuna anayefaa kufikiri kwamba huu ndio mwisho. Hakuna anayefaa kutufanya tujihisi kuwa na hatia, kwani tuna njia nyingine za kikatiba za kuchukua kupinga mambo yaliyofanywa na tume."

Kwa kusema hivyo, alionekana kugusia njia ya kuwaita wananchi kushiriki maandamano au mgomo kushinikiza mageuzi.

Wachanganuzi wamekuwa wakifuatilia msimamo wa Nasa na yanayojitokeza ni mambo mawili makuu ambayo huenda yanaufanya muungano huo kutoamini kwamba utashinda iwapo utawasilisha kesi kortini.

1. Ushahidi

Kuna uwezekano kwamba huenda muungano huu haujapata ushahidi wa kutosha wa kuhakikisha wanaweza kuwasilisha kesi yenye uzito mahakamani na kushinda. Kwa hilo, huenda hawataki kujiingiza katika mbio ambazo wanajua tayari watakuwa wameshindwa.

2. Uhuru wa mahakama

Upinzani tangu kushindwa kwenye kesi ya mwaka 2013, umekuwa ukiituhumu idara ya mahakama mara kwa mara kuwa ina ushirikiano na serikali. Hilo limekuwa likikaririwa kila wanaposhindwa kwenye kesi wanazowasilisha mahakamani.

Wakati pekee ambao Nasa walionekana kufurahishwa na mahakama ni pale waliposhinda kesi kuhusu kutangazwa kwa matokeo rasmi ya urais katika maeneo bunge. Walikuwa pia wameshinda uamuzi kuhusu zabuni ya kuchapishwa kwa karatasi za kura ingawa mwishowe Mahakama ya Rufaa ilibatilisha ushindi wao.

Kipindi hicho, serikali ya Jubilee ndiyo iliyokuwa inalalamika kuhusu mahakama. Bw Kenyatta na serikali yake waliamini kwamba maamuzi ya mahakama yangevuruga maandalizi ya uchaguzi.

Jambo la kushangaza ni kwamba upinzani wakati huo ulikuwa mstari wa mbele kuitetea mahakama na kumtaka Bw Kenyatta kuheshimu uamuzi na uhuru wa idara ya mahakama.

Upinzani ulikuwa pia unapinga kudumishwa kwa Jaji George Odunga kuwa miongoni mwa majaji ambao wangeshughulikia kesi za uchaguzi. Jubilee ilidai kwamba jaji huyo alikuwa na uhusiano na upinzani.

Jaji Mkuu David Maraga alishutumu sana Jubilee kwa kuingilia uhuru mahakama.

3. Historia ya kesi za uchaguzi Kenya na kwingineko

Baada ya kutupiliwa mbali kwa kesi ya kupinga kuchaguliwa kwa Bw Kenyatta mwaka 2013, Bw Odinga alisema hadharani kwamba hakuwa amefurahishwa na uamuzi wa mahakama. Alisema majaji walitumia vikwazo vya kiutaratibu kutupilia mbali sehemu kubwa ya ushahidi wake ambao ungeongeza uzito kwa kesi yao. Tangu wakati huo, amekuwa akikariri kwamba hakutendewa haki na hata kabla ya uchaguzi wa mwaka huu kufanyika, alikuwa ameweka wazi kwamba hangeenda kortini.

Tangu mwaka 1992, uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa ulipofanyika, kumewasilishwa kesi nyingi za kupinga matokeo lakini hakujakuwa na hata moja iliyofanikiwa kubatilisha matokeo.

Kupinga ushindi wa Moi

Wakati upinzani ulishindwa na Rais Daniel arap Moi mwaka wa 1992, jumla ya kesi sita ziliwasilsihwa mbele ya Mahakama Kuu, lakini zote, isipokuwa ile ya Kenneth Matiba, zilitupwa nje kwa misingi ya kutofuata utaratibu.

Matiba alikwenda mahakamani akidai kulikuwa na wizi mkubwa wakati wa uchaguzi kwa njia ya kujaza karatasi za kura kwenye masanduku ya kupigia kura kabla ya uchaguzi kufanywa.

Lakini kabla ya kesi hiyo kusikilizwa, Rais Moi alisema alikuwa na shaka na uhalali wa ombi la Matiba kwani saini iliyokuwa imetumiwa ilikuwa ya mke wake Matiba, Edith ambaye alikuwa amepewa mamlaka ya kuwa mwakilishi wa Matiba kisheria.

Matiba hakuweza kutia saini nyaraka za kesi kwa sababu alikuwa amepoteza uwezo wa kutumia mkono wake wa kulia na hakuweza kusoma kutokana na kiharusi alichokipata katika gereza la Kamiti, ambako alifungwa bila ya kufunguliwa mashtaka.

Wakati suala la saini liliposikizwa, Mahakama Kuu ilieleza kuwa sheria ilikuwa wazi kwamba Matiba alipaswa kutia saini kwenye nyaraka za kesi "yeye binafsi" na hivyo kesi ikatupiliwa mbali.

Kulikuwa na ombi jingine la John Harun Mwau - ambaye aliwania urais mwaka 1992 na ambaye aliiambia mahakama kuwa yeye ndiye mgombea pekee aliyeteuliwa kihalali kwa sababu wagombea wengine wote hawakuwasilisha orodha ya wafuasi waliowateua kwenye 'karatasi sahihi' .

Mwau, ambaye alikuwa amepata kura 6,499 pekee lakini alitaka kutangazwa rais kwa sababu sheria ilisema kwamba karatasi ya orodha ya wafuasi walioidhinisha mgombea lipaswa kuwa 'foolscap' ya kipimo cha 216mm x 343mm, ilhali wengine wote waliwasilisha karatasi ya 'A4' ya 21cm × 29.7cm.

Mahakama ilisema kwamba ingawa ombi la Mwau lilionekana kuwa la kutumia "werevu wa hali ya juu", halikuwa na msingi.

Kesi nyingine iliyowasilishwa ya kutaka matokeo ya uchaguzi wa urais kutupiliwa mbali ilikuwa baada ya uchaguzi wa 1997, ambao miongoni mwa walioshiriki uchaguzi huo kulikuwa na Mwai Kibaki, Kijana Wamalwa, Raila Odinga na Charity Ngilu.

Baada ya kugawanya kura zao, upinzani ulishindwa kumtoa Rais Moi mamlakani, ambaye alipata kura milioni 2.5 ikilinganishwa na mpinzani wake mkuu Bw Kibaki aliyepata kura milioni 1.9.

Bw Kibaki alipinga matokeo na kusema uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki.

Lakini kabla ya kesi hiyo kusikilizwa, Rais Moi alisema kuwa hakutumiwa ombi la kufika mahakamani yeye binafsi kulingana na Sheria za Uchaguzi wa Wabunge na Rais.

Kabla ya uchaguzi wa 1997, Sheria hiyo ilibadilishwa na Sheria ya 10 ya 1997, ambayo ilisema kwamba maombi ya kutilia shaka uhalali wa uchaguzi yalifaa yawasilishwe chini ya siku 28 baada ya kuchapishwa kwa matokeo ya uchaguzi. Kibaki alisema kuwa ilikuwa vigumu kumfikia Bwana Moi ndani ya ikulu. Mahakama ilitupilia mbali kesi hiyo.

Rais Kenyatta akihutubu baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais Ijumaa Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais Kenyatta akihutubu baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais Ijumaa

Mwaka 2013 baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangazwa mshindi, kuliwasilishwa kesi tatu mahakamani. Mbili zilikuwa za kupinga ushindi wa Bw Kenyatta.

Bw Raila Odinga, aliyekuwa wamewania urais kupitia chama cha ODM kwenye muungano wa Coalition for Reforms and Democracy (Cord) alitaka matokeo ya uchaguzi wa rais yatupiliwe mbali akisema kwamba kulitokea udanganyifu mkubwa na kasoro nyingi kwenye uchaguzi.

Miongoni mwa mengine, alizua maswali kuhusu sajili ya wapiga kura.

Shirika la Africa Centre for Open Governance (Africog) pia liliwasilisha kesi kortini kupinga uhalali wa ushindi wa Bw Kenya likisema kulikuwa na makosa mengi katika kusajiliwa kwa wapiga kura, kutambuliwa kwa wapiga kura vituoni na pia katika shughuli ya kuhesabu kura. Kesi hizo mbili zilitupiliwa mbali.

Mahakama ya Juu, ambayo chini ya Katiba ilikuwa inashughulikia masuala yaliyoibuka kuhusiana na uchaguzi wa rais, kwanza ilitupilia mbali kurasa 800 za ushahidi wa Odinga kabla ya mwishowe kuirusha nje kesi hiyo.

Katika uamuzi uliosomwa na Jaji Philip Tunoi, mahakama hiyo ilisema kwamba kukubali hati hiyo, na ushahidi mpya, wangekuwa wanawaonea waliotakiwa kujibu kesi hiyo ambao ni Issack Hassan, IEBC, Uhuru Kenyatta na William Ruto kwani muda ulikuwa umepita.

Kulikuwa na kesi ya tatu iliyowasilishwa na washirika wa Bw Kenyatta.

Kesi hii iliwasilishwa na Dennis Itumbi, Moses Kuria na Florence Sergon ambao walitaka ufafanuzi wa kuhusu iwapo kura zilizoharibika au kukataliwa zilifaa kuhesabiwa wakati wa kuamua idadi ya kura zilizopigwa na hivyo katika kuamua iwapo mgombea alipata asilimia 50 ya kura na zaidi. Mahakama iliamua kura zilizoharibika hazifai kutumiwa kufanya hesabu ya kura zilizopigwa.

Samahani, kisakuzi chako hakiwezi kuonesha ramani hii

Ingawa upinzani umesema wakati huu kwamba hautaenda kortini kupinga matokeo, hii haina maana kwamba Bw Kenyatta anaweza kutulia na kusubiri tu kuapishwa.

Kuna uwezekano kwamba kunaweza kukatokea shirika au mtu binafsi ambaye atawasilisha kesi ya kupinga kuchaguliwa kwa Bw Kenyatta.

Kesi hiyo itachukuliwa kwa uzito sawa na ule ambao ungepewa kesi ya kuwasilishwa na chama cha siasa kilichoshiriki uchaguzi au mgombea urais.

Bw Odinga anatarajiwa kutangaza hatua atakayoichukua Jumanne

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii