Wanajeshi wa Marekani waliokuwa na meli ya USS Fitzgerald kuadhibiwa

Damage to USS Fitzgerald, 18 June 2017 Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Meli hiyo ya USS Fitzgerald iliharibiwa sana

Jeshi la wanamanaji la Marekani limetangaza kwamba wanajeshi takriban kumi ambao walikuwa kwenye meli ya kivita ya USS Fitzgerald ilipogongana na meli nyingine wataadhibiwa.

Mabaharia saba waliokuwa kwenye meli hiyo walifariki dunia.

Meli hiyo ya kivita iligongana na meli ya mizigo ya Ufilipino katika eneo la bahari la Japan mwezi Juni.

Naibu mkuu wa shughuli za jeshi la wanamaji la Marekani Bill Moran amesema afisa mkuu wa meli hiyo pamoja na wanajeshi wengine wawili wa ngazi ya juu hawataruhusiwa tena kuhudumu katika meli hiyo.

Alisema jeshi la wanamaji limepoteza imani na uwezo wa watatu hao kuongoza.

Meli ya mizigo ya ACX Crystal iligongana na USS Fitzgerald mapema asubuhi 17 Juni karibu na Tokyo.

Shimo kubwa lilitoboka na maji yakaanza kuingia katika maeneo ya chini ya meli hiyo ya kivita.

Wanajeshi saba wa kati ya umri wa miaka 19 na 37 walifariki, na miili yao ilipatikana katika vyumba vyao baada ya wapiga mbizi kufikia maeneo ya meli hiyo yaliyokuwa yameharibiwa.

Afisa mkuu wa meli hiyo alikwama kwenye chumba cha nahodha kutokana na iliwabidi mabaharia watano kutumia nyundo kuuvunja mlango kumfikia.

Meli ya ACX Crystal iliharibiwa kidogo lakini hakuna aliyejeruhiwa kati ya mahabaria 20 waliokuwepo.

Uchunguzi bao unaendelea kuhusu ajali hiyo.

Sheria za ubaharia zinasema meli inafaa kuiondokea meli nyingine upande ambao meli hiyo ya kivita iliharibiwa, jambo linalozua uwezekano kwamba huenda meli hiyo ya Marekani ndiyo iliyokuwa na makosa.

Image caption Ramani ya safari ya meli hiyo ya Ufilipino na eneo ambalo meli hizo mbili ziligongana.

Mada zinazohusiana