Mshukiwa wa shambulio la Barcelona Younes Abouyaaqoub auawa

Barcelona Haki miliki ya picha AFP

Maafisa wa polisi ambao wamekuwa wakimsaka mshukiwa mkuu wa shambulio la kigaidi lililotekelezwa Alhamisi wiki iliyopita ambapo gari lilivurumishwa kwenye watu Barcelona wamempiga risasi mshukiwa mmoja magharibi mwa mji huo wa Barcelona.

Vyombo vya habari vinasema mshukiwa huyo alipigwa risasi eneo la Subirats, karibu na Sant Sadurní d'Anoia na alionekana kuvalia mkanda wa kujilipua.

Polisi wamethibitisha kwamba mshukiwa huyo Younes Abouyaaqoub, 22, ambaye alikuwa awali ametajwa kuwa mshukiwa aliyekuwa akisakwa kuhusiana na shambulio hilo la Las Ramblas ndiye aliyeuawa.

Taarifa kwenye vyombo vya habari zinasema mwanamume huyo alisema kwa sauti "Allahu Akbar" ("Mungu ni mkuu") alipokabiliwa na maafisa hao.

Operesheni hiyo ya polisi ilitekelezwa maili 25 (40km) kutoka Barcelona, ambako shambulio hilo la Las Ramblas liliua watu 13.

El Mundo wameripoti kuwa msako ulianzishwa baada ya polisi kupashwa habari kwamba mwanamume aliyeonekana kufanana na Abouyaaqoub alikuwa ameonekana katika kituo kimoja cha mafuta.

Abouyaaqoub alikuwa awali amedaiwa kuliteka gari hilo na kisha kuliendesha kwa nguvu kupitia kizuizi cha maafisa wa polisi na baaaye akaliacha gari hilo.

Polisi walikuwa wanashuku kwamba huenda alikuwa amefanikiwa kuingia Ufaransa.

Haki miliki ya picha Catalan police/El Pais

Dereva wa gari hilo Pau Pérez, 34, kutoka Vila Franca, alipatikana ameuawa kwa kudungwa kwa kisu akiwa kwenye kiti cha nyuma cha gari hilo.

Mwanamume huyo ndiye mwathiriwa wa 15 wa shambulio hilo la Barcelona na jingine lililotekelezwa eneo la Cambrils muda mfupi baadaye ambapo mwanamke alifariki baada ya gari kuvurumishwa kwenye eneo la wapita njia.

Washukiwa watano wa ugaidi waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi eneo hilo la Cambrils.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Watu wameacha ujumbe wa kuwakumbuka waliouawa Las Ramblas

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii