Shughuli za uokoaji zaendelea Houston, Marekani

Marekani
Image caption Houston inavyoonesha madhara ya dhoruba Harvey

Mshauri wa masuala ya usalama wa Rais Trump, Tom Bossert, amesema kwamba shughuli za uokozi bado zinaendelea Houston, baada ya dhoruba ya kitropiki ya kimbunga Harvey.

Bwana Bossert amesema watu elfu moja wameathiriwa vibaya na mafuriko hayo. Amethibitisha pia kuwa Ikulu ya Marekani itawasilisha ombi la dharula katika bunge la Congress kuomba fedha za ziada ili kuweza kukabiliana na janga hilo.

Rais Donald Trump amekwisha changia kiai cha dola milioni moja kutoka katika mapato yake binafsi katika kusaidia mfuko wa maafa. Lakini pia amekwisha kuutembelea mji wa Rockport, ulioko Texas, Naye makamu wa raisi Mike Pence, amewaambia wakaazi wa maeneo hayo kwamba utawala wa serikali uko pamoja nao wakati wote.

Nje ya mji wa Houston moto ulikuwa ukiendelea kuwaka ndani ya mafuriko kwenye kiwanda kimoja cha kemikali.

Shirika la Ulinzi wa Mazingira la Marekani limehakikisha kwamba hakuna kemikali za sumu katika moshi unaoenea.

Mpaka sasa watu thelathini wamepoteza maisha tangu kimbunga Harvey kilichotokea pwani kama kimbunga kikali.