Vikwazo vya Marekani vyaathiri utalii wa Korea Kaskazini

Sekta ya utalii inakua kwa kasi Korea Kaskazini
Image caption Sekta ya utalii inakua kwa kasi Korea Kaskazini

Zuio la Marekani juu ya raia wake kuingia nchini Korea Kaskazini limeongeza madhara,wakati huu ambapo kumeibuka hali ya kusuguana baina ya mataifa hayo mawili.

Zuio hilo lilitolewa baada ya mwanafunzi kutoka Marekani Otto Warmbier kufariki punde tu alipoachiliwa kutoka gerezani Korea Kaskazini.

Marekani imesema ni muhimu kufanya hivyo kwa lengo la kuwaweka salama wananchi wake.

Kwa raia yeyote wa Marekani atakayekiuka sheria hiyo, atakumbana na adhabu ikiwemo kunyanganywa hati ya kusafiria.

Marekani imesema itaruhusu tu wananchi wake kusafiri kwenda Korea Kaskazini kwa sababu muhimu ikiwemo uandishi wa habari ama utoaji wa misaada ya kibinaadam.

Waandaaji wa ziara za kitalii wanasema kuwa takribani wamarekani 1,000 hutembelea Korea Kaskazini kila mwaka.

Wageni wengine ambao huingia Korea Kaskazini kwa wingi kama watalii ni raia wa China.

Siku ya Alhamis, waendeshaji wa biashara ya utalii waliwaondoa raia wa Marekani wa mwisho waliokuwa Pyongyang.

Image caption Takriban watalii 5,000 kutoka nchi za Magharibi kuitembelea Korea Kaskazini kila mwaka

Simon Cockerell, mkuu wa shirika la kitalii la Koryo Tours, ameiambia BBC kwamba anatarajia kupungua zaidi kwa watalii katika ukanda huo kupita awali.

''Licha ya kwamba katazo hili litawaathiri raia wa Marekani, lakini linatuma ujumbe fulani ambao unaashiria kuwazuia watu wa nchi nyingine kutotembelea Korea Kaskazini'' alisema.

Otto Warmbier alikamatwa na kufungwa gerezani mwaka 2016 kwa kudaiwa kufanya njama za kufanya upelelezi akiwa kwenye hoteli moja wakati akiwa likizo.

Aliachiliwa na kupelekwa kwa familia yake mwezi June lakini alikua dhaifu sana na kufariki baadae, huku chanzo cha kifo chake kikiwa bado hakijulikani.

Marekani inasema kwamba takriban raia 16 wa nchi yake wameshikiliwa Korea Kaskazini kwa muongo mmoja sasa, huku watatu kati yao wakiwa bado kizuizini.

Image caption Otto Warmbier alizungumza na waandishi wa habari 2016 na kukana kuhusika na tuhuma za kipelelezi

Wengi wao ni wamisionari,waandishi wa habari na Maprofesa.

Marekani imeilaumu Korea Kaskazini kwa kuwashikilia raia wake mara kwa mara na kuwatumia kama chambo ya kusuluhisha migogoro ya kumiliki silaha za nyuklia.

Wiki hii Korea Kaskazini ilitishia tena kurusha makombora yake ya nyuklia kwenye kisiwa cha Marekani cha Guam, huku ikianza kwa jaribio la kurusha kombora kwenye bahari ya Pacific kwa upande unaopakana na Japan.