Kimbunga Irma chasababisha uharibifu mkubwa Caribbean

Picha zimeonesha mafuriko makubwa kisiwa cha Saint Martin, 6 Septemba Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Picha zimeonesha mafuriko makubwa kisiwa cha Saint Martin

Kimbunga kilichopewa jina Irma kimeharibu majumba na kusababisha mafuriko makubwa katika visiwa vinavyomilikiwa na Ufaransa katika eneo la Caribbean.

Majumba manne "imara zaidi" katika visiwa vya Saint Martin, ambavyo humilikiwa na Ufaransa na Uholanzi, yameharibiwa, waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Gérard Collomb amesema.

Uharibifu mkubwa umeripotiwa katika maeneo ya kisiwa hicho ambayo humilikiwa na Uholanzi.

Kimbunga hicho kimeorodheshwa kuwa cha ngazi ya tano, ngazi ya juu zaidi.

Kimbunga hicho kina upepo unaovuma kwa kasi inayofikia 295km/h (185mph).

Kimbunga hicho chenye nguvu zaivi kuwahi kuripotiwa kutoka Bahari ya Atlantiki katika kipindi cha mwongo mmoja kiligonga kwanza visiwa vya Antigua na Barbuda, kabla ya kuelekea Saint Martin na Saint Barthélemy - kisiwa maarufu sana kwa watalii kutoka Ufaransa ambacho hufahamika sana kama St Barts.

Ubashiri wa Kituo cha Taifa cha Vimbunga cha Marekani unasema kitakuwa "kimbunga hatari sana".

Kimbunga hicho kinatarajiwa kupitia maeneo ya kaskazini ya visiwa vya Virgin Islands Jumatano, na kisha kipitie karibu au kaskazini kidogo mwa kisiwa cha Puerto Rico. Baadaye, kitafululiza na kupitia karibu na au kaskazini mwa pwani ya Jamhuri ya Dominika siku ya Alhamisi.

Haki miliki ya picha Vimbunga

Maelfu ya watu wamehamishwa kutoka kwa maeneo yaliyo hatarini.

Wakazi wamefika madukani kununua chakula, maji na dawa vya kujihifadhia.

Viwanja vya ndege katika visiwa vingi eneo hilo vimefungwa.

Katika eneo la Key West katika jimbo la Florida, Marekani, watu wameamrishwa kuhama. Kimbunga hicho kinatarajiwa kufika eneo hilo wikendi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kimbunga cha Irma kinavyoonekana kutoka anga za juu 11:30 GMT Jumatano

Watu takriban 40,000 huishi upande wa Ufaransa visiwa vya Saint Martin, na inakadiriwa idadi sawa huishi upande wa Uholanzi.

Kuna wakazi zaidi ya 9,000 visiwa vya St Barts.

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza hali ya dharura Florida, Puerto Rico na visiwa va Marekani vya US Virgin Islands, na idara za serikali ya taifa zitasaidia kuwahamisha wakazi na katika juhudi za uokoaji.

Baadhi ya maeneo ya Texas na Louisiana yanakabiliana na uharibifu uliotokana na Kimbunga Harvey mwishoni mwa Agosti.

Kufikia sasa haijabainika Kimbunga Irma kitakuwa na uharibifu kiasi gani Marekani bara.

Kimbunga kingine kwa jina Jose kimejiunga nyuma ya irma na kinatarajiwa kukomaa kabisa baadaye Jumatano.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii