Wengi wa wanaojiunga na Boko Haram na al-Shabab hukosa elimu ya kidini

Mwanafunzi Maiduguri, Nigeria, on 12 May 2012 Haki miliki ya picha AFP
Image caption Boko Haram, jina ambalo maana yake ni kuwa "Elimu ya magharibi ni haramu", wamekuwa wakishambulia shule kaskazini mwa Nigeria

Wengi wa vijana kutoka Afrika ambao huingizwa katika makundi yenye itikadi kali huwa "wana ufahamu mdogo sana au hawafahamu hata kidogo" vitabu vya kidini na ufasiri wake, utafiti wa Umoja wa Mataifa umebaini.

Utafiti huo, wa kwanza wa aina yake Afrika, ulishirikisha watu 500 waliokuwa wamejitolea kwa hiari kujiunga na makundi ya wanamgambo yakiwemo al-Shabab na Boko Haram.

Utafiti huo uligundua kwamba kutafuta kazi huwa ni "hitaji la muhimu zaidi wakati wa kujiunga na kundi" lenye itikadi kali.

Ripoti ya utafiti huo inasema hatua kutoka kwa serikali huwa mara nyingi ndiyo sababu ya mwisho inayowashawishi vijana kujiunga na makundi hayo.

Wengi wa waliohojiwa walisema walikuwa hawana furaha maisha yao ya utotoni na hawakutunzwa au kuangaliwa vyema na wazazi wao.

Watafiti kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) walizungumza na makurutu waliojiunga na makundi hayo Kenya, Nigeria, Somalia, Sudan, Cameroon na Niger wakati wa kuan daa ripoti hiyo.

Al-Shabab ngome yake ni Somalia lakini mara kwa mara hutekeleza mashambulio ya kigaidi kenya.

Boko Haram nao asili yao ni Nigeria lakini wameenea hadi nchi jirani za Niger na Cameroon.

Watafiti hao pia waliwahoji watu waliokulia katika mazingira sawa na waliojiunga na makundi hayo, lakini hawakubali kuingia katika makundi hayo yenye itikadi kali.

Kwa kutumia maelezo waliyopata, wanasema kupokea "angalau miaka sita ya mafunzo ya kidini (mfano katika Madrasa) , kumebainika huwa hunapunguza uwezekano wa mtu kujiunga na makundi ya itikadi kali kwa hadi 32%".

Haki miliki ya picha AFP
Image caption UN inakadiria kwamba watu 33,300 barani Afrika walipoteza maisha yao kutokana na mashambulio ya wanamgambo wa itikadi kali kati ya 2011 na mapema mwaka 2016

Wengi hushawishiwa kujiunga na makundi hayo baada ya kukutana na wanachama wa makundi hayo "ana kwa ana" badala ya kupitia mtandaoni kama ilivyo nje ya Afrika.

Ripoti hiyo inasema wengi wa wanaojiunga na makundi hayo huwa wanatoka maeneo ya mipakani ambayo wameathirika kutokana na jamii zao kutengwa kwa muda mrefu.

Mauaji ya jamaa au kukamatwa kwa jamaa au rafiki mara nyingi huwa jambo linalochochea watu kujiunga na makundi hayo, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Asilimia 70 ya waliohojiwa walisema hilo au aina nyingine ya hatua inayochukuliwa na serikali huwa jambo la mwisho linaloshawishi watu kujiunga na kundi la wanamgambo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mwanajeshi wa kundi linalounga mkono serikali la Ras Kimboni akishika doria Somalia

Uingiliaji kati ngazi ya mashinani ndiyo njia pekee ya kuzuia vijana kuingizwa katika makundi ya itikadi kali, watafiti hao wa UNDP wamesema.

Wanapendekeza "mikakati inayoongozwa na jamii yenye lengo la kuimarisha utangamano katika jamii" na "kuongeza usemi wa viongozi wa kidini mashinani ambao huhimiza watu kuvumiliana".

"Tarishi... huwa na umuhimu zaidi sawa na ujumbe," anasema mkurugenzi wa UNDP barani Afrika Abdoulaye Mar Dieye.

Huwezi kusikiliza tena
Wanawake waliofanywa watumwa wa ngono na al-Shabab

"Sauti hiyo ya kuaminika mashinani ina umuhimu sana pia katika kupunguza hisia za kujihisi kutengwa, hisia ambazo zinaweza kumfanya mtu aingizwe kwenye makundi yenye itikadi kali kwa urahisi."