Kenyatta: Tutatumia Bunge kumuondoa Odinga madarakani akishinda

Uhuru Kenyatta, 10 March 2013 Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Uhuru Kenyatta aliingia madarakani mara ya kwanza 2013,

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema mpinzani wake katika uchaguzi mkuu mpya utakaofanyika mwezi ujao akifanikiwa kushinda chama chake kitamuondoa madarakani muda mfupi baadaye kupitia bunge.

Uchaguzi mpya utafanyika tarehe 17 Oktoba baada ya matokeo ya uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti kufutiliwa mbali na Mahakama ya Juu.

Rais Kenyatta alikuwa ametangazwa mshindi akiwa na zaidi ya kura 1.4 milioni kumzidi Bw Odinga lakini kiongozi huyo wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) alipinga ushindi wake mahakamani.

Kampeni zimekuwa zikishika kasi nchini humo viongozi wa chama cha Jubilee chake Bw Kenyatta na muungano wa Nasa wakijibizana hasa kuhusu Tume ya Uchaguzi (IEBC) ambapo Nasa wanataka tume hiyo ifanyiwe mabadiliko kwanza kabla ya uchaguzi kufanyika.

"Hakuna cha kuogopa kama anavyosema William (Ruto). Hata Raila akichaguliwa, niambie atatawala nchi ya kenya kwa njia gani. Vipi, Jubilee tulivyo sasa. Katika seneti muhula uliopita tulitatizika kwa sababu ya idadi ya wabunge, leo hii tukiwa na maseneta 41, tunaweza kuendesha shughuli seneti bila kuwa na mwanachama hata mmoja wa Nasa. Hatuwahitaji," amesema.

"Leo hii katika Bunge, tukiwa na wabunge zaidi ya mia mbili na ishirini na kitu, tumepungukiwa na wabunge 13 pekee tuwe na wingi wa theluthi mbili, hii ina maana kwamba tunaweza hata kubadilisha katiba bila kuwa na mbunge wa Nasa."

"Atafanya nini, hata mkimpatia kura zote, atafanya nini? Anaweza kufanya nini? Hata akichaguliwa, tuna fursa Bunge, katika kipindi cha miezi miwili mitatu hivi, tumemtoa."

Kwa mujibu wa katiba nchini Kenya, Rais anaweza kuondolewa madarakani iwapo atabainika kutokuwa na uwezo kimwili na kiakili kuongoza.

Anaweza pia kuondolewa madarakani iwapo atakiuka sana katiba au atekeleze makosa ya jinai chini ya sheria za kitaifa au kimataifa.

Muungano wa upinzani Nasa umeshutumu vikali tamko la Bw Kenyatta na kusema halina busara.

"Bwana Uhuru Kenyata/ Jubilee, usijidanganye wewe na Wakenya, hauna idadi ya kutosha ya kumuondoa Raila madarakani au rais yeyote yule. Soma kifungu 145 cha katiba," aliandika Seneta wa Bungoma Moses Wetangula, mmoja wa viongozi wakuu wa Nasa.

Kiongozi mwingine wa muungano huo Musalia Mudavadi ambaye ni makamu wa rais wa zamani pia ameshutumu tamko la Bw Kenyatta.

Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Bw Odinga

Kando na kutishia kumuondoa madarakani Bw Odinga iwapo atashinda, Rais Kenyatta alipokuwa anahutubu ikulu ameushutumu upinzani kwa kutishia kususia kikao cha kufunguliwa rasmi kwa mabunge yote mawili.

Bw Kenyatta amesema mabunge yote mawili yanaweza kuendelea na shughuli zake bila kutegemea wabunge wa Nasa.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii