Las Vegas: Muuaji huenda alilenga tamasha lililohudhuriwa na mabinti wa Obama

Suspected gunman - undated image Haki miliki ya picha Paddock family
Image caption Picha ya Stephen Paddock aliyetekeleza mauaji Las Vegas

Mshambuliaji ambaye aliwaua watu 58 kwenye tamasha eneo wazi Las Vegas na kisha kujiua alikuwa amekodisha vyumba ambavyo vilikuwa karibu na maeneo ambayo kulikuwa kunaandaliwa matamasha awali, wachunguzi wanasema.

Tamasha moja ambalo huenda alilenga kushambulia lilihudhuriwa na mabinti wa Rais mstaafu Barack Obama, Malia na Sasha.

Stephen Paddock alikuwa amekodi chumba wakati wa tamasha ya Life is Beautiful mjini Vegas wiki moja kabla yake kutekeleza mauaji hayo.

Sasa, imebainika kwamba mhasibu huyo mstaafu alikuwa pia amekodi vyumba vilivyokuwa karibu na maeneo mengine yaliyokuwa yanaandaliwa matamasha miji ya Chicago na Boston.

Wachunguzi bado hawajabaini lengo la Paddock katika kutekeleza mauaji hayo.

Mwanamume aliyejitambulisha kwa jina Stephen Paddock alikuwa amekodi chumba kwenye hoteli ya Blackstone mjini Chicago, wakati tamasha ya Lollapalooza ilikuwa ikifanyika katika jiji hilo la jimbo la Illinois.

Lakini hakukaa katika chumba hicho.

Msemaji wa hoteli hiyo amesema bado hawajathibitisha iwapo ni Stephen Paddock aliyetekeleza mauaji.

Miongoni mwa watu waliohudhuria tamasha hiyo mwezi Agosti ni mabinti wa Rais mstaafu Barack Obama, Malia na Sasha.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Tamasha ya Lollopalooza, imekuwa ikifanyika Grant Park mjini Chicago tangu 2003

Taarifa kwamba muuaji huyo alikodi vyumba hivyo zimeibuka baada ya afisa wa polisi wa wilaya ya Clark Joseph Lombardo kufichua kuwa Paddock alikuwa pia ameomba atengewe chumba kingine cha hoteli wiki moja kabla ya mauaji ya Jumapili.

Chumba hicho kilikuwa katika jumba refu la ghorofa la Ogden, ambalo lilikuwa karibu na tamasha nyingine ya wazi ya muziki, Life is Beautiful, ambapo waliotumbuiza ni pamoja na Muse, Lorde na Chance the Rapper.

Hayo yakijiri, The Boston Globe wameripoti kuwa Paddock pia alitafuta taarifa mtandaoni kuhusu Fenway Park na Kituo cha Sanaa cha Boston, wakimnukuu afisa mmoja wa serikali.

Maeneo yote mawili yaliandaa matamasha ya wazi karibuni.

Wachunguzi zaidi ya 100 wanatafuta habari kuhusu maisha ya Paddock ambaye ameelezwa kama "mtu hatari aliyetatizika kiakili", ili kubaini lengo la mauaji yake.

Lombardo amesema Paddock aliishi "maisha ya usiri, na kufikia sasa mambo mengi kumhusu hayajaeleweka."

Mpenzi wa muuaji huyo amesema hakuwa na habari zozote kwamba alipanga kutekeleza mauaji.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii