Uchaguzi Kenya: Tume ya IEBC yasema wagombea wote watashiriki

Image caption Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati

Tume ya uchaguzi na mipaka nchini kenya IEBC imesema kuwa wagombea wote 8 waliowania urais tarehe 8 mwezi Agosti mwaka huu, watawania tena kwenye uchaguzi mpya ambao utafanyika tarehe 26 mwezi huu.

Tarehe mosi mwezi Septemba mahakama ya juu nchini Kenya ilifuta matokeo ya uchaguzi ulioandaliwa tarehe nane mwezi Agosti.

Mahakama hiyo kisha ikaamrisha kuwa uchaguzi mpya ufanyike ndani ya siku 60.

Sasa IEBC imetoa taarifa ikisema kuwa wagombea wote 8 walioshiriki, watashiriki tena uchaguzi huo licha ya awali kutangaza kuwa ni Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa muungano wa NASA Raila Odinga ndio wangeshiriki uchaguzi mpya.

Jana Jumanne Raila odinga alitangaza kujiondoa kwenye kinyanganyiro hicho cha tarehe 26, akidai kuwa IEBC haijafanya mabadiliko yanayostahili kwa mujibu wa uamuzi uliotolewa na mahakama.

IEBC inatangaza hayo baada ya mgombea urais kupitia chama cha Third Alliance, Ekuro Aukot, kwenda mahakamani na kutaka kushirikishwa kwenye uchaguzi huo wa tarehe 26, ambapo ombi lake lilikubaliwa na mahakama.