Sheikh Ponda apewa siku 3 kujisalimisha kwa polisi Tanzania

Sheikh Ponda apewa siku 3 kujisalimisha kwa polisi Tanzania
Image caption Sheikh Ponda apewa siku 3 kujisalimisha kwa polisi Tanzania

Maafisa wa polisi nchini Tanzania wamempatia katibu mkuu wa baraza la mashirika ya kiislamu siku tatu kujisalimisha kwa madai ya kutoa matamshi ya uchochezi kulingana na gazeti la The Citizen nchini Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi yake, afisa mkuu wa polisi anayesimamia maeneo maalum bwana Lazaro Mambosasa amesema kuwa Sheikh Ponda alifanya makosa hayo siku ya Jumatano wakati wa mkutano na wanahabari .

The Citizen limenukuu kamanda huyo wa polisi akisema kuwa matamshi yaliotolewa na kiongozi huyo wa dini yaliidharau serikali .

Bwana Mambosasa ameongezea kwamba ni sharti ajisalimishe kati ya Alhamisi na Jumamosi la sivyo atajipata katika matatizo.

''Ninamshauri Sheikh Ponda kujisalimisha kwa sababu hata akitoroka haitamsaidia kwa sababu tutamkamata'', alisema Mambosasa.

Aliongezea: Alijua kwamba anavunja sheria, wakati alipotoa matamshi ya uchochezi na sasa ajiandae kukabiliwa kisheria.

Kiongozi huyo wa dini amekuwa akijikuta katika mikono ya sheria mara kwa mara kila anapotoa matamshi yake.

Mada zinazohusiana