Mzozo Zimbabwe: Jeshi 'lachukua udhibiti wa chumba cha habari- ZBC'

Magari ya kijeshi yanaonekana yakidhibiti barabara za mji mkuu Harare jana Jumanne Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Magari ya kijeshi yanaonekana yakidhibiti barabara za mji mkuu Harare jana Jumanne

Mapema leo Jumatano alfajiri, milio ya risasi na milipuko imesikika karibu na makazi ya kibinafsi ya Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe, katika mji mkuu Harare.

Mashuhuda wanaoishi karibu na kasri la Mugabe lililoko maeneo ya Borrowdale, Harare, wameiambia shirika la habari la kimataifa AFP, kuwa, mwendo wa saa nane usiku wa kuamkia leo jumatano saa za Zimbabwe, milio zaidi ya 40 ya risasi zilisikika kwa muda wa dakika tatu ama nne hivi.

Baadaye mizinga mizito ikasikika kote katika mji mkuu Harare, baada ya wanajeshi kutumwa kupiga doria katika barabara za mji huo mkuu, na duru zinasema kuwa wamechukua udhibiti wa kituo kikuu cha habari cha serikali- ZBC.

Taarifa zinasema kuwa huenda kuna njama za kuipindua serikali ya Rais Robert Mugabe mwenye umri wa miaka 93, na amabaye amekaa mamlakani tangu mwaka 1980.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Emmerson Mnangagwa, awali alisema kuwa chama tawala kimetekwa nyara

Hayo ni baada ya tetesi kusema kuwa mkuu wa majeshi alitishia "kuchukua mamlaka ya nchi" baada ya kufutwa kazi kwa makamu wa Rais mwenye ushawishi mkubwa nchini humo Emmerson Mnangagwa juma lililopita.

Chama tawala nchini Zimbabwe cha ZANU PF lilimshtumu vikali Jenerali Constantine Chiwenga na kutishia kumshitaki kwa kosa la uhaini baada ya kutoa matamshi hayo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kamanda mkuu wa Jeshi nchini Zimbabwe Jenerali Constantino Chiwenga alionya kuwa huenda jeshi likachukua uongozi wa taifa hilo

Kwa sasa vifaru vya kijeshi vinaonekana nje ya chumba kikuu cha habari cha taifa Zimbabwe Broadcasting Corporation- ZBC.