Tanzania: Kukohoa kohoa Unguja sasa kwaweza kuwatia wanaume matatani

Baadhi ya wanawake hukumbwa na vitendo vya udhalilishaji wanapopita njiani na wanapokuwa kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu
Image caption Baadhi ya wanawake hukumbwa na vitendo vya udhalilishaji wanapopita njiani na wanapokuwa kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu

Vijana wanaodaiwa kukosa maadili mkoani Kaskazini Unguja, Tanzania wakijihusisha na vitendo vinavyotafsiriwa kuwa udhalilishaji wa utu wa mwanamke, watajikuta matatani iwapo wataendelea na vitendo hivyo.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa mjini Magharibi Unguja Hassan Nasir Ally amekemea vitendo hivyo alivyovitaja kuwa ''shambulio la aibu''

''Mwanamke akipita pengine maumbile yamejazajaza ukaanza kukohoa mh mh hilo ni shambulio la aibu, tutakukamata tukupeleke mahakamani".

Akizungumza na BBC kamanda Hassan ametaja kuwa kumekuwepo na ripoti kuhusu udhalilishaji katika eneo lake.

''Tuna wastani wa ripoti tano kwa wiki kuhusu udhalilishaji wa wanawake mkoa wa Kaskazini Unguja, tuliona tunahitaji kupambana na vitendo hivyo''

''Kuna ndugu zetu , watoto wetu, Mama zetu unakuta wana maumbo makubwa unakuta mtaani kuna vijana wasio na maadili, hawana adabu wamezoea kukohoa na kuzomeazomea wanapowaona wanawake wanapita mbele yao wanafanya wakiwa hawajui kama ni kosa la jinai jeshi la Polisi linafanya kazi ya kulinda utu wa mwanamke.Tutawashitaki kwa sheria ya kulinda wanawake na watoto.''

Haki miliki ya picha Zanzinews
Image caption Polisi imesema itapambana na vitendo vya mashambulizi ya aibu dhidi ya wanawake na watoto

Idadi ya kesi za udhalilishaji wa wanawake imeongezeka kwa mujibu wa Takwimu zilizotolewa na chama cha waandishi wa habari wanawake TAMWA-ZANZIBAR ambapo kwa miezi mitatu ya mwanzo wa mwaka huu 2018 tayari kumeripotiwa kuwepo kwa kesi 44 za udhalilishaji dhidi ya wanawake, watoto na vijana wa kiume vilevile takwimu hizo zinaonyesha kwamba mkoa wa Kaskazini Unguja unaongoza kwa vitendo vya udhalilishaji.

Mwaka 2017 zilifunguliwa kesi 105 za udhalilishaji wa wanawake pamoja na watoto visiwani zanzibar ambapo kati ya kesi hizo, 57 zilikamilika na kutolewa hukumu.

Asilimia 81% ya kesi zote zilizosajiliwa mwaka jana zilikuwa za kubaka.Mzuri Issa ambaye ni mkurugenzi wa TAMWA Visiwani Zanzibar alieleza kuwa hali si shwari

''Vitendo vya ukatili vinafedhehesha kwa miaka mingi. Zanzibar iliangaliwa kuwa yenye ustaarabu wa hali ya juu na yenye kufuata misingi ya dini lakini vitendo hivi vimekuwepo kwa muda mrefu na vinaongezeka''

Wakati wananchi katika ngazi tofauti wakilalamikia sheria kuwa haziko rafiki kwa waathirika wa vitendo vya udhalilishaji, sasa watakaotuhumiwa kudhalilisha wanawake na watoto wakifikishwa mahakamani hawatapewa dhamana na wakikutwa na hatia adhabu imeongezeka kwa kila ngazi ya mahakama na hii ni kwa mujibu wa chapisho lililotolewa na TAMWA la Mwezi Aprili mwaka huu.