Sheria ya uhalifu wa kimitandao Kenya: Kenyatta aidhinisha sheria inayotoa adhabu ya dola 50,000 kwa habari feki

Kenyatta akitia saini mswada Haki miliki ya picha PSCU

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameidhinisha Mswada wa Sheria za Uhalifu wa Kompyuta na Mtandaoni wa 2018 kuwa Sheria, hatua itakayotoa adhabu kali kwa watakaopatikana na makosa ya mtandaoni.

Sheria hiyo inatoa adhabu ya faini ya Sh5 milioni (dola 50,000 za Marekani) au kifungo cha miaka miwili jela, au adhabu zote mbili, kwa atakayepatikana na kosa la uenezaji wa habari za uzushi.

Mtu atakayepatikana na kosa la kueneza taarifa ambazo zinaweza kuzua taharuki au kuzua vurugu atafungwa jela zaidi ya miaka kumi.

Sheria hiyo inatarajiwa kuathiri utendakazi wa wanahabari, vyombo vya habari, watumiaji wa mitandao ya kijamii, wanablogu na watu wengine wanaotumia kompyuta na mitandao.

Lakini je ni kweli sheria hiyo mpya itakandamiza uhuru wa kujieleza?

Wakati wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa wanahabari mapema mwezi huu, mwenyekiti wa Chama cha Wahariri Kenya Bw Churchill Otieno alikuwa amesema sheria hiyo inaweza kutumiwa kuminya uhuru wa wanahabari.

Alieleza kuwa kifungu kinachozungumzia uenezaji wa habari za uzushi au uongo kinaweza kutumiwa vibaya na maafisa wa dola.

Huwezi kusikiliza tena
Je ni kweli sheria mpya ya Uhalifu wa Mtandao itakandamiza uhuru wa kujieleza Kenya ?

Kiongozi wa zamani wa Chama cha Wanasheria Kenya Apollo Mboya amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kifungu hicho kinaweza kuwapa watawala 'uhuru' wa kukandamiza vyombo vya habari.

Shirika la kimataifa la kutetea uhuru wa wanahabari Committee to Protect Journalists (CPJ) nalo lilikuwa limemhimiza Rais Kenyatta kutoidhinisha mswada huo kuwa sharia.

Makundi ya kueteta haki za binaadamu wameishutumu sheria hiyo na kuitaja kuwa ya hatari.

Shirika la Article 19 East Africa, linataja makosa kadhaa yalio mapana ambayo yana adhabu kali zinazoweza mwishowe kuzuia uhuru wa kujieleza katika mitandao Kenya.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Makundi ya kueteta haki za binaadamu wameishutumu sheria hiyo na kuitaja kuwa ya hatari.

Sheria hiyo bado inawacha wazi masuala kadhaa, kama vile kusambazwa kwa picha za utupu kwa dhamira ya kumchafulia mtu jina, udukuzi, na utumiaji haramu wa data binafsi - licha ya kushutumiwa pakubwa shughuli za kampuni ya Cambridge Analytica katika uchaguzi mara mbili wa urais nchini.

Kampeni ya kuwasaka wanaoeneza habari za uongo Afrika mashariki

Sheria mpya Kenya ya kupambana na uhalifu katika mtandao inafuata nyingine kama hiyo katika mataifa ya Afrika Mashariki kuwaadhibu watu wanaosambaza 'habari za uongo'na kutoa adhabu kali kwa wahalifu wa mitandaoni.

Hali sio tofuati sana katika nchi jirani ya Tanzania ambapo maafisa hivi maajuzi walitangaza sheria mpya zinazowahitaji wanablogu kulipa .

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais John Magufuli ameunga mkono sheria hiyo Tanzania

Serikali inasema inataka kulilinda taifa hilo dhidi ya 'uongo' unaosambazwa katika mitandao, licha ya kwamba wakosoaji wanaiona hatua hiyo kama njia ya kukandamiza uhuru wa kujieleza.

Rais John Magufuli amesema ananuia kukabiliana na anachokitaja kuwa ni 'ugonjwa'.

Hatahivyo mahakama kuu nchini ilizuia utekelezaji wa sheria hiyo mnamo Mei 5 baada ya kundi la wanaharakati na wawakilishi kutoka vyombo vya habari nchini kuzusha pingamizi.

Iwapo sheria hiyo itapita kesi iliyopo kotini, inatoa adhabu ya faini isiyo chini ya $2,000 au kifungo kisicho chini ya mwaka mmoja au yote mawili kwa wahalifu watakaopatikana na makosa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Museveni alipendekeza kuidhinisha kodi ya kutumia mitandao ya kijamii

Nchini Uganda, serikali ya rais Yoweri Museveni imezuia mipango ya kuidhinisha kodi ya kutumia mitandao ya kijamii baada ya wizara ya fedha kusema inahitaji kushauriana kuhusu vipi mpango huo wa kodi utaweza kuidhinishwa.

Museveni alipendekeza watu watozwe kodi kwa kutumia mitandao ya kijamii Facebook na WhatsApp, akisema kodi itakayokusanywa italisaidia taifa hilo kukabiliana na athari za Olugambo [uvumi]".

Wakosaji wanasema nia ya kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 73 ni kukandamiza vyombo vya habari na wale wanaopinga mpango wake wa kuwania tena urais katika uchaguzi mkuu wa 2021.

Serikali yake ilifunga mitandao ya kijamii wakati wa uchaguzi mkuu mnamo 2016.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii