Jeshi la Congo laua raia 49

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limeua raia 49 baada ya kuuteka uwanja wa ndege upya mjini Mbandaka kutoka kwa waasi mapema mwezi huu.

Walioshuhudia wameliambia kundi la kutetea haki za bindamau, Asadho kuwa watu tisa waliokamatwa miezi mitatu kabla, walishutumiwa kuwa ni waasi na kuuawa kikatili.

Kundi hilo pia limegundua kuwa miili ya watu 33 iliachwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.

Shambulio hilo lililotokea kwenye uwanja wa ndege, na kuzua mapigano juu ya haki za uvuvi, limesababisha vifo vya wafanyakazi wawili wa shirika la Umoja wa Mataifa.

Jeshi la Kongo lina sifa mbaya la kuhusika na ukatili, wizi na kubaka watu wanaotakiwa kuwalinda.

Maelfu ya waliokuwa waasi wamejiunga na jeshi hilo kufuatia makubaliano kadhaa ya amani.