Uchaguzi wa Sudan waendelea kuzua utata

Kura za hesabiwa Sudan
Image caption Wasimamizi wa tume ya uchaguzi Sudan kwenye kituo cha kupiga kura.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha pili kwa ukubwa huko Sudan Kusini ameieleza BBC kuwa kulikuwa na vitendo vingi vya ukiukwaji wa sheria katika uchaguzi wa kihistoria uliofanyika hivi karibuni.

Lam Akol, mkuu wa SPLM-Democratic Change, na viongozi wa vyama vingine vinane vya Sudan Kusini wameamua kwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi.

Salvir Kiir, kiongozi wa chama cha Sudan People's Liberation Movement (SPLM), alipata ushindi wa asilimia 93 ya kura zote za kusini.

Mpinzani wake pekee alikuwa Bw Akol - ambaye anachukuliwa kuwa anawakilisha maslahi ya serikali kuu ya Sudan Kaskazini.

Malalamiko

Bw Akol alimweleza mwandishi wa BBC, James Copnall, mjini Khartoum kuwa anataka mahakama zibatilishe na kutengua matokeo ya kusini kwasababu uchaguzi ulitawaliwa na udanganyifu na kwamba matokeo hayo hayawakilishi maoni ya wananchi.

"Ukweli uko wazi kabisa," alieleza.

"Mgombea [Bw Kiir] kupata asilimia 93 ya kura ni jambo halijawahi kutokea katika mchakato wa kidemokrasia.

"Pia ni ushahidi kuwa kuna udanganyifu mkubwa."

Bw Akol alidai kuwa wakati wa upigaji kura majeshi ya usalama ya SPLM yalichukua udhibiti wa vituo vya kupigia kura, waliwatisha na kuwanyanyasa wapiga kura, na kukamata wawakilishi wa vyama vya upinzani.