Mpinzani wa Sudan Kusini ahoji uchaguzi

Kiongozi wa chama cha pili kwa ukubwa Sudan ya Kusini ameiambia BBC kuwa kulikuwa na udanganyifu mkubwa katika uchaguzi wa hivi karibuni.

Lam Akol, kiongozi wa chama cha SPLM-Democratic Change, na viongozi wa vyama vengine vinane vya kusini wameamua kupinga matokeo hayo kwa kufikisha malalamiko ya mahakamani.

Salva Kiir, kiongozi wa Sudan People's Liberation Movement (SPLM), ameshinda kwa asilimia 93 ya kura upande wa kusini.

Mpinzani wake pekee alikuwa Bw Akol, anayeonekana kuwa mwakilishi kutoka kaskazini.

Bw Akol amemwambia mwandishi wa BBC James Copnall mjini Khartoum kwamba anataka mahakama ibatilishe matokeo ya upande wa kusini kutokana na udanganyifu na matokeo kutoendana na maoni ya umma.

Amesema " Ukweli uko wazi."

"Mgombea [Bw Kiir] kupata asilimia 93 ya kura zote haijwahi kutokea katika mchakato mzima wa kidemokrasia."

"Ni wazi kuwa kumefanyika udanganyifu wa hali ya juu."

Bw Akol amedai majeshi ya usalama ya SPLM yalivamia vituo vya uchaguzi, yaliwatishia wapiga kura, na kuwakamata mawakala wa vyama vya upinzani.