Mwandishi wa habari Tunisia aachiliwa

Taoufik Ben Brik
Image caption Taoufik Ben Brik

Mwandishi wa habari anayeipinga serikali ameachiliwa huru baada ya kutumikia kifungo cha miezi sita gerezani kwa kosa la kushambulia.

Taoufik Ben Brik, mkosoaji mmarufu wa Rais Zine El Abidine Ben Ali, amekuwa akidai mara zote kuwa kukamatwa kwake kunahusishwa na siasa.

Baada ya kuachiwa, Bw Ben Brik ameiambia BBC ataendelea kumpinga Rais wa nchi hiyo.

Bw Ben Ali amekuwa madarakani kwa muda wa miaka 23 na si mwepesi kustahamili upinzani, lakini maafisa wanakataa kuwa Bw Ben Brik alisingiziwa.

Bw Ben Brik anayejulikana kwa ukosoaji kwa tashtiti ameiambia BBC ataandika juu ya mambo yaliyomsibu gerezani, pamoja na matukio yaliyosababisha yeye kukamatwa, bila kujali Rais wa nchi hiyo atamfanya nini.

Amesema, "Ben Ali hatoacha". "Nadhani nikendelea kuandika, ana uwezo wa kunipiga risasi."

Mwezi Novemba 2009, alitiwa kizuizini kwa kumshambulia mfanyabiashara wa kike hadharani.

Amesema, alikuwemo kwenye chumba cha mahabusu na wafungwa wengine 20 ambapo chakula walichopewa hakifai hata kuwapa 'mbwa' au 'panya'

Bw Ben Brik amesisitiza atahudhuria siku ya kuadhimisha uhuru wa vyombo vya habari duniani mjini Paris tarehe 3 Mei.