Kenya yapinga ripoti ya ajali ya ndege

Waokoaji wakiwa eneo la ajali ya Kenya Airways nchini Cameroon.
Image caption Ndege hiyo aina ya Boeing 737 ilikuwa safarini kutoka Cameroon kwenda Kenya.

Mzozo umeibuka kati ya Kenya na Cameroon kuhusu ripoti ya uchunguzi wa chanzo cha ajali ya ndege ya Kenya Airways iliyoanguka mwaka 2007.

Tarehe 5 mwezi Mei mwaka 2007, ndege ya Kenya Airways, ilianguka mara tu baada ya kuondoka katika uwanja wa Douala, Cameroon na kusababisha vifo vya watu wote 114 waliokuwemo ndani. Ripoti hiyo inasema makosa ya rubani wa ndege hiyo huenda ndiyo yaliyosababisha ajali hiyo. Lakini serikali ya Kenya kupitia Naibu waziri wa uchukuzi, Amos Kimunya, inasema haikubaliani na ripoti hiyo.

Ripoti inaeleza kuwa naibu rubani alikuwa kijana mwenye umri wa miaka 23 na kwamba huenda kulikuwa na mgongano na kutoelewana kati ya kijana huyo na rubani mkuu aliyekuwa na umri wa miaka 52.

Serikali ya Kenya pamoja na wakuu wa shirika la ndege la Kenya Airways waliandaa kikao na wanahabari na kusema hawakubaliani na baadhi ya madai yaliyomo kwenye ripoti hiyo.