Kenya yataka mapatano na Dubai

Ramani kuonyesha Kenya na Dubai.
Image caption Kenya inajaribu kupata suluhu kuwapunguzia kero wananchi wake wanaotaka kuingia Dubai.

Waziri wa mambo ya nje wa Kenya, Moses Wetangula yuko Dubai kujaribu kutuliza mvutano baada ya ndugu wa familia ya kifalme ya Imarati kurejeshwa nyumbani kwa kushukiwa kuwa magaidi.

Watu hao wanne walikuwa mapumzikoni katika pwani ya Mombasa wakati wa Pasaka, wakati maafisa wa uhamiaji walipowahoji kwa saa kadhaa kabla ya kufukuza nchini humo.

Umoja wa Imarati za Kiarabu ulijibu mashambulizi kwa kuongeza masharti ya visa - na kusema raia wa Kenya wenye shahada ya chuo kikuu pekee ndiyo wataruhusiwa kuingia nchini humo.

Marufuku

Marufuku huyo iliwaathiri wafanyabiashara wengi, ambao kwa kawaida hununua bidhaa zao kutoka Dubai.

Magari yaliyotumika na nguo ni baadhi ya bidhaa zinazosafirishwa kwa kiasi kikubwa kutoka Dubai kuingia Kenya.

Waziri wa mambo ya nje, Bw Wetangula na ujumbe wake waliwasili Dubai siku ya Jumatatu, lakini mazungumzo hayakuzaa matunda, badala yake muda wa majadiliano ukaongezwa.

Juma lililopita, naibu waziri wa mambo ya nje, Richard Onyonka aliomba radhi kupitia matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC kwamba maafisa husika walifanya makosa.

Kwa mujibu wa gazeti la Standard, zaidi ya raia 37,000 wa Kenya wanaishi, hasa Dubai.