Ugiriki yazidi kulemewa na madeni

Waandamanaji kupinga kuyumba uchumi Ugiriki.
Image caption Wananchi wamekuwa wakiandamana kupinga hatua za serikali ya Ugiriki kuokoa uchumi wa nchi hiyo.

Ugiriki imeendelea kuwa na wasi wasi wa uchumi wake kuanguka, hali iliyosababisha masoko ya hisa kuyumba na kuathiri mataifa yanayotumia sarafu ya Euro.

Gharama za kukopa zimeongezeka kwa kiasi kikubwa huku kiwango cha riba ya dhamana za Ugiriki zikipanda mpaka kufikia takriban asilimia 19.

Wakati huo huo, Ureno imechukua hatua kuwahakikishia wawekezaji, baada ya wasi wasi kuongezeka kuwa mgogoro wa Ugiriki unaweza kuenea katika nchi nyingine zinazotumia sarafu ya Euro lakini zina uchumi dhaifu.

Msaada

Kiongozi wa Ujerumani, Bi Angela Merkel, atafanya mazungumzo kuhusu matatizo hayo wakati akitafakari endapo achangie kuokoa uchumi wa nchi hizo.

Hata hivyo, Bi Merkel anafahamu kwamba hatua ya kukubali kuikoa Ugiriki inaweza isipokelewe vizuri na wapiga kura wake - wengi wao wanadai kuwa Ugiriki ilitakiwa isiruhusiwe kujiunga na sarafu ya Euro.

Masoko ya hisa ya Ulaya yaliporomoka kwa kiasi kikubwa Jumatano asubuhi, kutokana na madeni ya Ugiriki kuonekana kuwa hayalipiki, ingawa mchana masoko yaliimarika kidogo.

Katika hatua nyingine, sarafu ya euro ilishuka thamani kufikia kiwango cha chini zaidi dhidi ya dola, kabla ya kuinuka kwa asilimia chache.