Obama ajaribu kusaidia Ugiriki

Sarafu ya Euro
Image caption Rais Obama anajaribu kusaidia ufumbuzi wa tatizo la Ugiriki.

Rais Barack Obama wa Marekani amefanya mazungumzo ya simu na Chansella wa Ujerumani, Angela Merkel, kujadili matatizo ya kiuchumi yanayoikumba Ugiriki, huku kukiwa na onyo kuwa yanaweza kusambaa kote barani Ulaya.

Taarifa kutoka Ikulu ya White House imesema suala hilo linapaswa kupewa umuhimu mkubwa. Ripoti hiyo imesema rais Obama na Bi Merkel wamekubaliana kuwa Ugiriki ilihitaji kuchukua hatua za dharura, kuomba usaidizi kutoka kwa shirika la fedha duniani IMF na Muungano wa Ulaya.

Shirika hilo limesema mpango wa Ulaya wa kuinusuru Ugiriki unahitajika kwa haraka, kwa sababu hali hiyo inaendelea kuwa mbaya zaidi.

Siku ya Jumatano hadhi ya Uhispania ilishushwa na shirika linalochunguza ubora na uwezo wa nchi kulipa madeni yake, Standard & Poor's.