Maafisa wa ngazi ya juu Kenya mahakamani

Maafisa kumi wa zamani wa serikali nchini Kenya wanafikishwa mahakamani kwa tuhuma za ufisadi juu ya ununuzi wa kipande cha ardhi kwa ajili ya kutenga sehemu ya makaburi.

Washitakiwa hao wanatuhumiwa kwa kutumia zaidi ya dola milioni tatu kwa kununua eneo hilo, ambalo thamani yake ilikuwa asilimia 10 tu ya kiasi kulichotajwa, na pia eneo hilo halikuwa na hati.

Watu hao 10, ambao ni pamoja na aliyekuwa karani wa halmashauri ya jiji la Nairobi na afisa mwingine wa ngazi ya juu wa serikali za mitaa walikamatwa siku ya Jumatano.

Wahisani wamelaani vikali serikali ya Kenya kwa kutopambana na ufisadi.

Watu hao walikamatwa na maafisa wa tume ya kupambana na rushwa ya Kenya (Kacc).

Msemaji wa Kacc, Nicholas Simani amesema uchunguzi huo umeonesha "wizi uliopangwa vizuri na maafisa walioidanganya halmashauri ya jiji".

Amesema ardhi hiyo iliyonunuliwa haifai kwa ajili ya kutengwa kwa ajili ya makaburi.

Inadaiwa kuwa kipande cha ardhi hiyo kilichopo katika wilaya ya Machakos, kilinunuliwa kwa shilingi milioni 283, wakati thamani yake ilikuwa shilingi milioni 24.

Watu wengine tisa pia wanachunguzwa kuhusiana na sakata hilo.