Maafisa wa Kenya wakanusha mashitaka

Maafisa kumi wa zamani wa ngazi za juu nchini Kenya, wamekana mashitaka ya ufisadi kuhusiana na ununuzi wa eneo kwa ajili ya makaburi.

Maafisa hao wa zamani wanatuhumiwa kulipa dola milioni 3.6, fedha za walipa kodi kwa ajili ya kununua ardhi hiyo, ambayo thamani yake ni asilimia 10 ya fedha zilizolipwa.

Image caption John Gakuo aliyekuwa karani wa jiji la Nairobi amekana mashitaka

Imeelezwa kipande cha ardhi hiyo hakina hati kamili za umiliki.

Watu hao 10, ambao ni pamoja na aliyekuwa karani wa jiji la Nairobi John Gakuo na afisa mwingine aliyekuwa na wadhifa mkubwa katika serikali za mitaa, walikamatwa siku ya Jumatano.

Wahisani wameishitumu vikali serikali ya Kenya kwa kushindwa kupambana na ufisadi.

Mwandishi wa BBC jijini Nairobi, Odhiambo Joseph anasema washukiwa hao walifikishwa mahakamani chini ya ulinzi mkali baada ya kulala rumande.

Maafisa hao kumi wamesomewa mashitaka 11 ya udanganyifu na matumizi mabaya ya ofisi, kabla ya kuachiliwa huru kwa dhamana.

Mawakili wa washukiwa wengine wanne wanaotuhumiwa kwa mashitaka kama hayo wamesema wateja wao wanapanga kujisalimisha wiki ijayo.

Wanasheria pamoja na wafanyabiashara ni miongoni mwa watu waliofikishwa mahakamani.

Image caption Jiji la Nairobi

Msemaji wa tume ya kupambana na ufisadi nchini Kenya Nicholas Simani amesema uchunguzi huo umeonesha "wizi uliopangwa vizuri na maafisa walioidanganya halmashauri ya jiji".

Mamlaka za huko zinasema eneo hilo la ardhi ambalo lina majabali na halifai kwa ajili ya makaburi.

Inadaiwa kuwa eneo hilo lipo katika wilaya ya Machakos, na lilinunuliwa kwa shilingi za Kenya milioni 283, wakati thamani yake halisi ni shilingi milioni 24.