Mkutano wa Madagascar kufanyika A.Kusini

Mahasimu wa kisiasa Madagascar.
Image caption Mahasimu wa kisiasa Madagascar.

Mazungumzo ya amani yanayokusudiwa kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini Madagascar yanaanza upya huko Afrika Kusini. Kiongozi wa sasa wa nchi hiyo Andry Rajoelina, ameieleza BBC kuwa hatarajii kuafikiwa kwa mkataba wowote kati yake na rais aliyeondolewa madarakani Marc Ravalomanana.

"Kuna pengo kati ya hali halisi na makubaliano ambayo tayari yamefikiwa," Rajoelina aliwaleza waandishi wa habari, na kuongeza kuwa mazungumzo yataanza upya mjini Pretoria.

"Nadhani kuna uwezekano mdogo wa kuunda serikali ya Umoja wa kitaifa na ufumbuzi lazima upatikane kwa njia nyingine," alisema.

Jeshi la nchi hiyo ambalo lilimsaidia Bw Rajoelina kutwaa mamlaka ya nchi hiyo, limempa hadi mwisho wa mwezi huu kumaliza mgogoro huo.

Mwandishi wa BBC mjini Pretoria amesema, Bw Ravalomanana anataka kurejea nyumbani, kwa masharti asifunguliwe mashtaka kuhusiana na vifo vya watu 130 wakati wa maandamano yaliyomng'oa mamlakani mwaka uliopita.

Mazungumzo hayo ni mwendelezo wa mikutano kati ya makundi yanayowaunga mkono Ravalomanana na Rajoelina, na marais wastaafu Didier Ratsiraka na Albert Zafy.