Maafisa wakiri mashitaka Rwanda

Maafisa wawili nchini Rwanda wanaodaiwa kuunda kundi la kigaidi kwa lengo la kuhujumu nchi wamekiri mashitaka dhidi yao.

Maafisa hao Luteni Kanali Tharcisse Mbiturende na Luteni Kanali Habiyakare Noel wamekiri mashitaka hayo ambayo ni pamoja na madai ya kushirikiana na mwanasiasa Ingabire Victoire.

Ingabire Victoire ametangaza kuwania kiti cha urais katika uchaguzi utakaofanyika baadaye mwaka huu nchini Rwanda.

Image caption Ingabire Victoire amehusishwa na kundi la FDLR

Upande wa mashitaka umedai maafisa hao walikuwa wanatumukia jeshi la Rwanda kabla ya kujiunga na kundi la FDLR kwa lengo la kuvuruga usalama.

Ingabire Voctoire ambaye ni mkosoaji wa serikali alikuwa akitajwa sana, mapema wakati kesi ikianza.

Uhusiano wa karibu

Mwendesha mashitaka ameonesha ushahidi wa barua pepe, unaodhihirisha uhusiano kati ya maafisa hao wa kijeshi na Bi Ingabire. Aidha ushahidi wa mikutano iliyofanyika mjini Kinshasa na fedha walizotumiana umewasilishwa katika mahakama ya Gasabo, mjini Kigali.

Wakikiri mashitaka hayo, washukiwa hao wamekiri kuwa na uhusiano wa karibu na bi Ingabire na kusema aliwataka waunde kundi jipya, lakini walikamatwa kabla ya kutekeleza hilo.

Upande wa utetezi umetaka kujua kwa nini washukiwa hao walikamatwa mwezi Septemba mwaka jana, lakini wamefikishwa mahakamani miezi saba baadaye. Mwendesha mashitaka amesema utaratibu wa kisheria umefuatwa.