Licha ya kesi Kagame atembelea Marekani

Rais wa Rwanda Paul Kagame amewasili Marekani, akipuuza kesi iliyofunguliwa nchini humo dhidi yake kutokana na mauaji ya Marais wawili wa Kiafrika mwaka 1994.

Bw Kagame alizungumza katika sherehe zilizofanyika mjini Oklahoma kuwatunukia shahada wanafun zi wa Kinyarwanda.

Image caption Kagame alituhumiwa na Ufaransa kwa mauaji ya Marais wawili wa zamani wa Afrika

Wajane wa waliokuwa viongozi wa Burundi na Rwanda, ambao vifo vyao viliibua mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, wamesema Bw Kagame aliamuru ndege yao itunguliwe.

Bw Kagame amekanusha tuhuma hizo. Mawakili waliofungua kesi hiyo hawakuweza kuwasilisha nyaraka za kisheria wakati wa ziara yake.

Rais Kagame alikuwa mzungumzaji mkuu wakati wa sherehe hizo zilizofanyika katika Chuo Kikuu cha Kikristo cha Oklahoma Christian University siku ya Ijumaa.

Alipeana mikono na wanafunzi wa Rwanda pamoja na wasomi wengine na alisema elimu itakuwa ni njia pekee ya kuisaidia nchi yake kuendelea kuondokana na maumivu ya mauaji ya kimbari.

Hata hivyo aliondoka mapema kabla sherehe hazijamalizika na hakutamka lolote juu ya kesi iliyofunguliwa. Watu walioshuhudia wamesema alikuwa amezungukwa na walinzi.

Fidia

Wajane wa Marais wa zamani Juvenal Habyarimana wa Rwanda na Cyprien Ntaryamira wa Burundi hawaishi Marekani, lakini kwa mujibu wa mawakili wao waliamua kufungua kesi ya mauaji mjini Oklahoma kwa sababu ya uhusiano alionao Bw Kagame na Chuo Kikuu hicho. Wanadai fidia inayofikia dola za Marekani milioni 350.

Image caption Mjane wa Rais wa zamani wa Rwanda Agathe, anadai fidia kwa serikali ya Rwanda

Msemaji wa Chuo Kikuu hicho ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba Bw Kagame amekwenda chuoni hapo kwa heshima ya wanafunzi na hatajihusisha na masuala ya "siasa ya nchi yake".

Mwaka 1994 Bw Kagame alikuwa kiongozi wa waasi akiongoza chama cha Rwandan Patriotic Front (RPF), kilichoiangusha serikali iliyokuwa madarakani.

Ndege iliyowachukua Rais Habyarimana ambaye alikuwa ni Mhutu na Bw Ntaryamira iliangushwa tarehe 6 mwezi wa Aprili mwaka 1994. Serikali ya Wahutu wenye siasa kali iliwashutumu RPF kwa kuhusika na utunguaji wa ndege hiyo.

Muda mfupi baadae, wanaharakati waliweka vizuizi barabarani na kuanza maujia ya Watutsi na Wahutu waliokuwa na msimamo wa wastani kwa wakati mmoja. takriban watu 800,000 waliuawa wakati wa wimbi la mauaji hayo yaliyochukua siku 100.

Uhusiano na Ufaransa

Mara zote RPF imekuwa ikiwashutumu Wahutu wenye msimamo mkali kwa kuiangusha ndege ya Marais hao, ili kupata kisingizio cha kutekeleza mipango yao ya mauaji.

Bw Kagame pia alikuwa anatuhumiwa na Ufaransa kuhusika na utunguliwaji wa ndege hiyo.

Mapema wiki hii vyombo vya habari vya Ufaransa viliripoti kwamba jaji wa Paris anayechunguza kuangushwa kwa ndege hiyo, Marc Trevidic, alikuwa na mipango ya kuwatuma wataalam nchini Rwanda.

Jaji aliyechukua nafasi ya Bw Trevidic, Jean-Louis Bruguiere, ameituhumu RPF kwa kuitungua ndege hiyo na ametaka Rais Kagame akamatwe.

Hatua hiyo ilisababisha Rwanda kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Ufaransa. Serikali ya Rwanda pia imeishutumu Ufaransa kwa kuwaunga mkono watawala walioangushwa wa Kihutu.