Marekani yanusurika kulipuliwa

Times Square
Image caption Eneo la Times Square likiwa tupu baada ya polisi kugundua bomu la kutegwa ndani ya gari

Polisi mjini New York, Marekani wametegua bomu la kutegwa ndani ya gari lililokuwa limeegeshwa katika eneo lenye watu wengi mjini humo, Times Square.

Maafisa wa huko wamesema matanki ya gesi za kulipuka, fashifashi, petroli na kifaa cha kutega saa vimeondolewa kutoka ndani ya gari hilo.

Eneo ambalo gari hilo limepatikana, lina kumbi kadhaa za michezo ya kuigiza, limefungwa na kuzuia watu kuingia.

Rais wa Marekani Barack Obama na Meya wa New York Michael Bloomberg wamepongeza juhudi za idara ya polisi ya New York.

"Tuna bahati sana", Bw Bloomberg amewaambia waandishi wa habari. "Shukrani za pekee ziwaendee polisi na wakazi wa New York, kwani tumeepuka janga la kutisha" ameongeza meya huyo.