Ajali yaua watu 24 Afrika Kusini

Afrika Kusini
Image caption Ramani ya Afrika Kusini

Watu 24 wamefariki dunia na wengine 10 kujeruhiwa katika ajali ya basi nchini Afrika Kusini

Basi hilo lilikuwa linapita kwenye barabara kuu kuelekea Cape Town wakati dereva aliposhindwa kulidhibiti.

Shirika la habari la AFP limesema basi hilo lilipinduka katika jimbo la Western Cape takriban kilomita 150 kaskazini magharibi mwa mji huo.

Afrika Kusini ambayo ni wenyeji wa Kombe la Dunia mwezi Juni, wana rekodi mbaya ya usalama barabarani, huku maelfu wakiuawa kila mwaka.

Msemaji wa askari wa usalama barabarani wa jimbo hilo, Xenophone Wentzel ameliambia shirika la habari la AFP, "Dereva alishindwa kudhibiti basi, kisha likapita kwenye kizuizi, likapinduka na mwisho likaishia upande wa pili wa ilipokuwa ikielekea."

Amesema, baadhi ya waliojeruhiwa wamepelekwa hospitali kwa gari la wagonjwa na helikopta.

Bw Wentzel amesema ajali hiyo ilitokea asubuhi na mapema na watoto ni miongoni mwa waliofariki dunia.

Amesema pia basi hilo la mtu binafsi lilipigwa marufuku kutumika na idara ya askari wa usalama barabarani wa jimbo jirani la Eastern Cape kwa kuwa halikuwa na sifa ya kutumika barabarani.