Mtuhumiwa wa ugaidi Marekani ashtakiwa

Eneo la Times Square mjini New York ambalo shambulizi lilitibuliwa
Image caption Eneo la Times Square mjini New York

Raia huyo wa Marekani mwenye asili ya Pakistan ameshtakiwa kwa kosa la ugaidi na kujaribu kutumia silaha za maangamizi katika shambulio lililotibuka la kutumia bomu lililotegwa katika gari.

Maafisa wa Marekani wamesema Faisal Shahzad, mwenye umri wa miaka 30, amekiri kupata mafunzo ya kutengeneza mabomu nchini Pakistan.

Bw. Shahzad alikamatwa akiwa ndani ya ndege iliyokuwa ikielekea Dubai, katika uwanja wa ndege wa JFK mjini New York, siku mbili baada ya bomu hilo kupatikana.

Awali, Rais Barack Obama aliwashauri raia wa Marekani wasiruhusu kutawaliwa na na hofu kwa sababu ya tukio hilo.

Bw Obama alisema tukio hilo ni kumbusho la nyakati tunazoishi na kuahidi kwamba haki itatendeka katika kushughulikia kesi hiyo.

Inaaminika kuwa Faisal Shahzad alinunua gari aina ya SUV ambalo lilipatikana limebeba bomu iliyotengenezewa nyumbani.

Licha ya jina lake kuongezwa katika orodha ya watu wasiotakiwa kusafiri, jumatatu iliyopita, Bw Shahzad alinunua tiketi katika shirika la ndege la Emirates na kufanikiwa kupita vizuizi vya ukaguzi vya usalama katika uwanja wa JFK.

Familia ya mtuhumiwa huyo inasemekana kutoka katika mji wa Peshawar, kaskazini mwa Pakistan. Eneo hilo ni ngome ya kundi la Taleban.

Bw. Shahzad alioa mke kutoka Peshawar miaka miwili iliyopita.