Urusi yaiokoa meli yake kwa maharamia

Marshal Shaposhnikov
Image caption Meli ya Marshal Shaposhnikov

Majeshi ya Urusi yamewaokoa mabaharia waliopo kwenye meli ya Kirusi iliyotekwa na maharamia wa Kisomali katika pwani ya Yemen.

Majeshi katika meli ya kivita Marshal Shaposhnikov waliifuata meli ya Moscow University iliyokuwa na mabaharia 23 kwa helikopta.

Wakati majeshi hayo yakifanya hivyo, maharamia hao wakaanza kufyatua risasi, iliyochochea kuwepo na kurushiana risasi kutoka pande zote mbili.

Majeshi hayo ya Kirusi yakaelekea kwenye meli hiyo ya Kirusi, na kuwaokoa mabaharia wake waliokuwa wamejifungia kwenye chumba maalum.

Mwandishi wa BBC mjini Moscow, Richard Galpin amesema maharamia 10 wamekamatwa. Kanali Alexei Kuznetsov, msemaji wa wizara ya ulinzi wa Urusi amesema maharamia hao kwa sasa wanashikiliwa kwenye meli hiyo.

Taarifa zinasema, watapelekwa Moscow kukabiliana na mashitaka.

Image caption Ramani ya Somalia

Kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa kuwa mmoja miongoni mwa maharamia hao aliuawa wakati wa harakati hizo.

Msemaji wa kampuni ya meli ya Urusi inayomiliki meli hiyo, Novoship, ameliambia shirika la habari la Reuters, “ Maharamia wameiachilia meli, mabaharia wote waliokuwepo wako hai na salama.”

“Wakati wa harakati hizo zilizochukua zaidi ya saa 20, maharamia hawakufanikiwa kumchukua hata baharia mmoja mateka.”

Uamuzi wa kuikomboa meli hiyo ulifanyika huku wakitambua “Kwamba mabaharia walikuwa salama na maisha pamoja na afya zao hazikuwa katika hatari yeyote.” Novoship amesema.

Mwandishi wa BBC mjini Nairobi Will Ross amesema licha ya kuwepo meli za kivita kadhaa zikipiga doria kwenye bahari ya Hindi na ghuba ya Aden, ni mara chache kwa jitihada za kuokoa kufanyika pale maharamia wanapovamia meli kwa kuhofia kuathiri usalama wa mateka.

Lakini katika tukio hili, mabaharia walizima injini na kujifungia kwenye chumba maalum wenye mlango usio rahisi kufunguka.

Mwandishi huyo pia amesema, mbinu ya kukimbilia chumba hicho maalum kimefanikiwa kuzuia matukio mengine mawili ya awali.

Njia yenye shughuli nyingi

Meli hiyo ya Moscow University ilitekwa siku ya Jumatano katika ghuba ya Aden, kwenye pwani ya Yemen, ilipokuwa ikielekea China, ikiwa na zaidi ya tani 80,000 za mafuta ghafi yeneye thamani ya dola za kimarekani milioni 50.

Ghuba ya Aden ni njia inayopitiwa na meli nyingi sana duniani, Warusi, Wamarakeni na mataifa ya Ulaya wamesambaza majeshi ya majini katika eneo hilo baada ya kuwepo mashambulio na maharamia kwenye meli za kibiashara.

Hata hivyo, maharamia wanaripotiwa kushikilia zaidi ya meli za kigeni 20 wakiwemo takriban mabaharia 400.

Siku ya Jumatano meli ya Marshal Shaposhnikov ilipelekwa kuokoa meli hiyo iliyotekwa.