ANC yampa adhabu Julius Malema

Malema ameamrishwa kuomba msamaha na kujizuia kupandwa na hasira

Kiongozi wa kundi la Vijana la chama tawala Afrika Kusini cha ANC Julius Malema, ameamrishwa kuhudhuria vipindi maalum vitakavyoweza kumsaidia kujifunza kukabiliana na hasira.

Katika kikao cha nidhamu Malema aliomba msamaha hadharani pamoja na kutozwa faini ya dola 1,300 kwa kuchafulia sifa chama cha ANC.

Maafisa wa chama hicho walimpta Malema na hatia ya kumkosea heshima rais Jacob Zuma kwa kumkosoa hadharani kama kiongozi wa ANC.

Malema alitoa taarifa akiomba msamaha kwa kusababisha mgawanyiko ndani ya ANC.

Rais Jacob Zuma alimkaripia bwana Malema hadharani baada ya kumfurusha mwandishi mmoja wa habari wa BBC katika kikao cha wanahabari, na juu ya tabia yake ya kubagua watu kwa misingi ya rangi pamoja na kumuunga mkono rais wa Zimbabwe Robert Mugabe.

Chama tawala kimekuwa kikitaka kutatua tatizo la Malema kabla ya baraza kuu la Chama hicho kukutana mwishoni mwa wiki hii.