Sambo ainidhishwa Makamu Rais Nigeria

Image caption Bw Sambo ameidhinishwa na bunge kuwa Makamu Rais wa Nigeria.

Amadi Sambo sasa ndiye makamu wa rais wa Nigeria uteuzi ambao umeidhinishwa na wabunge wa nchi hiyo katika kikao kilichoshuhudia malumbano makali. Hatua hiyo ina maana kuwa Rais Goodluck Jonathan hatakuwa na upinzani mkali ndani ya serikali yake.

Bw Sambo hana ushawishi mkubwa wa kisiasa na huenda hilo likamwachia Goodluck Jonathan nafasi bora ya kugombea urais. Hata hivyo makamu huyo wa rais ni mtu ambaye amezingirwa na migogoro.

Katika kikao cha leo baadhi ya wabunge walijaribu kuchelewesha kuthibitishwa kwake kwa kupiga makelele na kulalamika huku wakitumia vipaza sauti bungeni.Katika jimbo lake la Kaduna, Bw Sambo, anaonekana kama mwanasiasa mdhaifu na ambaye hana uzoefu mkubwa.

Utawala wake katika jimbo hilo umehusishwa na ufisadi. Atakayerithi nafasi yake kama gavana wa Kaduna ni naibu wake ambaye ni mkristu hatua ambayo imesababisha hasira kwasababu jimbo hilo lina idadi kubwa ya waislamu. Baadhi ya wanasiasa wanaiona hatua hiyo kama juhudi za kutaka kuwapa wakristo udhibiti wa jimbo hilo.

Uhasama wa kidini sio jambo geni katika jimbo hilo la Kaduna na umewahi hata kusababisha mapigano na maelfu ya watu kuuawa.