Wanaume wapendanao hatiani Malawi

Wapenzi wa jinsia moja Malawi
Image caption Steven Monjeza na Tiwonge Chimbalanga

Mahakama nchini Malawi imewakuta na hatia wanaume wawili wa jinsia moja kwa kufanya vitendo kinyume cha umbile na vitendo vya aibu.

Steven Monjeza, 26, na Tiwonge Chimbalanga, 20, walikamatwa Desemba 2009 baada ya kusherehekea uchumba wao kabla ya harusi yao iliyopangwa kufanyika mwaka 2010.

Walikuwa gerezani kipindi chote hicho na huenda wakakabiliwa na kifungo cha miaka 14 jela.

Kukamatwa kwao kulizua malalamiko kutoka nchi za kimataifa na mjadala juu ya mapenzi ya jinsia moja ukaibuka nchini Malawi.

Jaji Nyakwawa Usiwa-Usiwa amewakuta na hatia wote wawili ambapo alisema ni kinyume na matendo ya kawaida. Hukumu yao inatarajiwa kutolewa Mei 20.

Mapenzi ya jinsia moja huchukiwa Malawi, nchi inayopinga kabisa vitendo hivyo kisheria.

Walikana kuhusika na mashitaka hayo na mawakili wao wamesema haki zao za kikatiba zimevunjwa.

Lakini kituo cha maendeleo ya watu (Cedep) na kituo cha haki za binadamu na kurekebisha tabia (CHRR) vimekuwa vikisihi mamlaka husika kulegeza msimamo juu ya wapenzi wa jinsia moja.

Mwandishi wa BBC Raphael Tenthani wa Blantyre amesema serikali nayo inashinikizwa na wafadhili kutoka nchi za magharibi kuhusiana na suala hilo.

Anasema shinikizo hilo kwa nchi maskini kama Malawi ambapo bajeti yake inategemea asilimia 40 kutoka kwa wafadhili, si jambo dogo.