Uingereza yatafakari sera zake Afghanistan

Image caption Liam Fox Waziri wa ulinzi wa Uingereza akiwa na mawaziri wenzake ziarani nchini Afghanistan.

Waziri wa Ulinzi wa serikali mpya ya Uingereza, Liam Fox, ambaye yuko ziarani nchini Afhanistan, amedokeza kuwa serikali yake inafikiria kubuni sera mpya kushughulikia vita vya Afghanistan.

Akihojiwa na gazeti moja la Uingereza kabla ya kwenda Afghanistan, Bw Fox alisema wanajeshi elfu kadha wa Uingereza, hawakwenda Afghanistan, kurekebisha sera za nchi inayoishi katika karne ya 13, bali wako huko kulinda maslahi ya taifa la Uingereza.

Waziri huyo wa Ulinzi, ambaye amefuatana na Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa, alisema anataka wanajeshi wa Uingereza kuondoka nchini Afghanistan kwa haraka iwezekanavyo.

Mawaziri hao watakutana na Rais Hamid Karzai na kamanda wa Marekani wa jeshi la kimataifa nchini humo.