Ajali ya ndege yaua 160 India

Eneo la ajali ya ndege nchini India.
Image caption Watu zaidi ya 150 wamefariki katika ajali iliyohusisha ndege ya Air India Express.

Ndege ya abiria, Air India Express, imeanguka na kuwaka moto karibu na uwanja mmoja kusini mwa India siku ya Jumamosi, na kuua watu 158, wengi wanaaminika kuwa raia wa India waliokuwa wakirejea nyumbani kutoka Dubai ambako walikuwa kibaruani.

Ndege hiyo aina ya Boeing 737-800 ilionekana kuteleza kutoka njia ya ndege katika uwanja wa Mangalore kwenye jimbo la Karnataka, kisha ikatumbukia msituni, mkurugenzi wa Air India, Anup Srivastava alieleza.

Watu wanane walisalimika miongoni mwa abiria na wafanyakazi 166 waliokuwa ndani ya ndege hiyo, alieleza. Miili isiyopungua 146 imepatikana,Mamlaka ya Safari za Anga imesema.

Televisheni za eneo hilo zilionyesha afisa wa zimamoto akiwa amebeba kilichoonekana kama mabaki ya mtoto huku moshi ukifuka kutoka mapande ya ndege. Miili iliyoungua kwa moto ilionekana imetapakaa msituni.

Abiria wote walikuwa raia wa India, afisa wa Air India alisema. Rubani alikuwa raia wa Serbia ambaye inasemekana alikuwa ana uzoefu mkubwa. Air India Express ni kampuni tanzu ya shirika linaloendeshwa na serikali, Air India.