Ethiopia yapiga kura

Bw Meles Zenawi
Image caption Bw Meles Zenawi

Raia wa Ethiopia wanapiga kura kwa mara ya kwanza tangu uchaguzi wa mwaka 2005 uliogubikwa na maandamano yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 200.

Misururu mirefu ya wapiga kura ilionekana kwenye vituo vya kupigia kura katika mji mkuu, Addis Ababa, kabla ya vituo kufunguliwa.

Waziri mkuu Meles Zenawi, washirika wa karibu wa nchi za magharibi ambao hupambana dhidi ya wapiganaji wa Somalia, wanapigania kuchaguliwa tena.

Lakini upinzani umeshaanza kulalamika juu ya uchaguzi huo.

Msemaji wa muungano wa upinzani, Medrek, amesema waangalizi wake wamekuwa wakitishiwa na kukamatwa katika baadhi ya maeneo nchini humo.

Nagesso Gidada ameliambia shirika la habari la AP, "Tunadhani hatutakubaliana na matokeo."

Msemaji wa serikali amepuuza madai hayo, akisema upinzani lazima ukubali kushindwa.

Mwandishi wa BBC Will Ross aliyopo Addis Ababa amesema vituo vya kupigia kura alivyotembelea kwenye mji mkuu vilikuwa na mpangilio mzuri, na wapiga kura wakijitokeza wa kutosha.

Upinzani umedai kulifanyika hila wakati wa uchaguzi wa mwaka 2005 ili kukipitisha chama tawala cha Bw Meles cha Ethiopian People's Revolutionary Democratic Front (EPRDF).

Bw Meles anatarajiwa kwa kiasi kikubwa kuchaguliwa tena, huku upinzani ukionekana kugawanyika na kutokuwa na mpangilio mzuri.

Marekebisho

Mwandishi wetu anasema sifa ya nchi ya pili yenye watu wengi barani Afrika inaangaliwa kwa makini kufuatia matukio ya mwaka 2005.

Mkuu wa bodi ya uchaguzi, Merga Bekana, amesema kutokana na kuwepo na marekebisho kwenye sheria za uchaguzi na mafunzo ya uhakika, matatizo ya uchaguzi uliopita yatarekebishwa.

Ameiambia BBC, " Hakuna namna yeyote ya kufanya udanganyifu, kwahiyo matokeo yako wazi safari hii. Tumejifunza mengi."

Kuna maelfu ya waangalizi kutoka nchini humo waliosambazwa maeneo mbali mbali japo wachache kutoka upinzani hawana imani nao.

Serikali ya Ethiopia imewazuia wafanyakazi wa balozi za kigeni kuwa kama waangalizi wa uchaguzi huo- haiwachukulii kama wataalamu wa uchaguzi na hawataki uhusiano wa kidiplomasi kuvurugika.

Umoja wa Ulaya una waangalizi 170- idadi kubwa mno ambapo mwandishi wetu anasema unaashiria namna umoja huo unavyouchuklia uchaguzi huo kwa uzito.

Takriban watu milioni 32 wamejiandikisha kuchagua wanachama 547 wa bunge la nchi hiyo, pamoja na madiwani.

Bodi ya uchaguzi ina mpaka tarehe 21 Juni kutangaza matokeo ya uchaguzi huo.