Kura zahesabiwa nchini Ethiopia

Idadi kubwa ya wapigaji kura walishiriki uchaguzi wa mwaka huu
Image caption Idadi kubwa ya wapigaji kura walishiriki uchaguzi wa mwaka huu

Shughuli ya kuhesabu kura za uchaguzi wa ubunge nchini Ethiopia inaendelea. Matokeo ya awali yanatarajiwa kuanza kutolewa hivi punde.

Uchaguzi huu unafanyika miaka mitano baada ya kura sawa na hizi ambazo zilikumbwa na machafuko na matokeo yake kuzozaniwa vikali. Wapigaji kura wengi wameripotiwa kushiriki katika uchaguzi wa mwaka huu.

Mwaka huu kama ilivyokuwa miaka mitano iliyopita upande wa upinzani umelalamika kuwa baadhi ya wafuasi wake walitolewa vitisho na kulazimika kupigia kura chama kinachotawala.

Waangalizi wa uchaguzi huu baado hawajatoa taarifa rasmi kuhusu mchakato mzima.

Hata hivyo mchunguzi mkuu wa uchaguzi kutoka Jumuiya ya Ulaya, Thijs Berman, amesema kuwa jumuiya hiyo itafanyia uchunguzi malalamiko yaliyotolewa kwa namna uchaguzi huo uliovyoendeshwa.

Naye msemaji wa serikali Berket Simon ameambia BBC kuwa madai hayo yametolewa na upinzani kwa nia ya kuharibu uchaguzi huo uliofanyika kwa amani.

Mwandishi wa BBC mjini Addis Ababa, Ken Mungai, anasema hali ya usalama imeimarishwa huku wengi wakitarajia chama tawala kuibuka na ushindi mkubwa.