Kesi ya maharamia wa Kisomali kuanza Uholanzi

Maharamia wa Kisomali

Kesi ya kwanza barani Ulaya inayohusisha watuhumiwa wa uharamia inaanza hii leo nchini Uholanzi. Wanaume watano wameshtakiwa kwa kujaribu kuiteka nyara meli ya mizigo katika ghuba ya Aden.

Walikamatwa mwaka jana wakati mashua yao ilipozingirwa na wanamaji wa Uholanzi waliokuwa wakishika doria pwani ya Somalia.

Wahukiwa hao wanakabiliwa na kifungo cha zaidi ya miaka 10 gerezani endapo watapatikana na hatia.

Watano hao walikamatwa mwezi Januari mwaka jana baada ya mashua yao kuzingirwa na wanamaji wa Uholanzi, wakati wakijaribu kuingia ndani ya meli moja ya mizigo kwa jina Samanyolu inayomilikiwa na kampuni moja kutoka Carebean.

Serikali ya Uholanzi ilitoa kibali kwa jumuiya ya Ulaya kwa watu hao kusafirishwa hadi nchini humo kutoka Bahrain ambapo walikuwa wakizuiliwa.

Mawakili wa washukiwa hao wamesema watapinga uhalali wa mahakama za Uholanzi kushughulikia kesi kuhusu makosa yanayodaiwa kutekelezwa nje ya nchi hiyo.

Mawakili hao pia wamesema washukiwa hao walikuwa wavuvi masikini ambao walikuwa wakijaribu kujikimu kimaisha.

Hata hivyo upande wa mashtaka umesema unatetea usalama wa meli ya nchi hiyo ambapo pia wasomali hao waliwafyatulia risasi mabaharia waliokuwa ndani na kuwazuilia kwa muda.