Mwimbaji wa Opera A Kusini afariki dunia

Mwimbaji nyota wa miondoko ya opera aliyechaguliwa na Nelson Mandela kuimba katika ufunguzi wa sherehe za Kombe la Dunia amefariki dunia kutokana na homa ya uti wa mgongo.

Image caption Siphiwo Ntshebe

Taarifa hiyo imetolewa na kampuni ya muziki inayosimamia kazi zake ya Epic.

Opera ni igizo inayoimbwa katika utamaduni wa Ulaya. Waigizaji hawasemi bali huimba maneno yao.

Kampuni hiyo ya muziki ya Epic imesema Siphiwo Ntshebe, 34, alilazwa hospitalini Port Elizabeth wiki iliyopita na kufariki dunia siku ya Jumanne.

Alitarajiwa kufanya onyesho la wimbo wake mpya uitwao 'Hope', ukiwa na maana 'Matumaini' katika ufunguzi wa sherehe hizo mjini Johannesburg Juni 11.

Mkuu wa kampuni hiyo ya Epic Nick Raphael amesema " Alikuwa na sauti nzuri na muziki wake ulikuwa wa kipekee katika miondoko na ujumbe wake wa matumaini na huruma."

Epic imesema Hope ilikuwa ni wimbo unaovuma kote ukiwa na "ujumbe maalum wa matumaini na huruma" ulioandikwa na kusemwa na Bw Mandela.

Wimbo na albamu wenye jina hilo hilo, ulitarajiwa kuanza kusambazwa ili kuenda sanjari na Kombe la Dunia.

Epic imesema hakuna uamuzi wowote uliotolewa wa aidha albamu hiyo isambazwe au la lakini familia ya Ntshebe imetaka nyimbo zake "zisikike kwa watu wengi inavyowezekana."

Mtayarishaji wa ufunguzi huo Lebo M amesema Ntshebe alikuwa "Mrithi wa kweli wa Kombe la Dunia, ametuacha mapema mno."

Mwandishi wa BBC Pumza Fihlani aliyopo mjini Johannesburg amesema Ntshebe hakuwa anajulikana sana Afrika Kusini- kuimba kwake katika ufunguzi wa Kombe la Dunia kungemtambulisha kwa umati mkubwa zaidi nchini mwake.

Ntshebe, aliyesoma katika chuo cha London Royal College of Music kati ya mwaka 2004 na 2007, alishiriki katika matamasha mbali mbali barani Ulaya.

Awali Bw Mandela alimsifia kwa kumwelezea kama " Kijana wa Afrika Kusini mwenye kipaji kikubwa, licha ya kupata changamoto nyingi, aliamua kufanya kazi kwa bidii ili kupata maisha bora."