Wagonjwa wa moyo wahofia ngono

Watafiti wa Marekani wanasema watu wengi waliowahi kupata maradhi ya moyo huepuka kujamiiana, wakihofia kuwa tendo hilo litawaua.

Watafiti hao wameuambia mkutano wa kimarekani wa masuala ya moyo kuwa asilimia kubwa ya wanaoepuka tendo hilo ni wale ambao madakatari wao walishindwa kuzungumza nao kuhusu suala hilo.

Image caption Wapendanao wakikumbatiana

Dr Stacey Tessler Lindau, aliyeongoza utafiti wa watu 1,700, amesema uwezekano wa kufa wakati wa kujamiiana "ni mdogo sana."

Shirika la British Heart Foundation limeunga mkono swala la madakatari kuzungumzia ngono na wagonjwa wao ili kuwapunguzia hofu.

Wataalamu wanasema ni salama kwa waliowahi kupata maradhi ya moyo kuanza kujamiiana tena baada ya kuweza kufanya mazoezi kiasi, kama vile kupanda ngazi chache.

Tendo la kujamiiana

Utafiti huo wa wanaume 1,184 na wanawake 576 waliokumbwa na maradhi ya moyo waliulizwa kuhusu kujamiiana kabla na baada ya kupata mshtuko wa moyo.

Walifanyiwa tathmini mwezi mmoja baada ya kupata maradhi hayo ya moyo, na tathmini nyingine ikafanywa baada ya mwaka mmoja.

Wanaume, waliokuwa na wastani wa umri wa miaka 59, walikuwa na nafasi kubwa ya kuoa kuliko wanawake, waliokuwa na wastani wa umri wa miaka 61.

Wanaume nao walionekana kushiriki zaidi katika tendo la kujamiiana kabla ya kupata maradhi hayo ya moyo.

Lakini hata baada ya kugundua tofauti hizo, wagonjwa waliopewa maelekezo ya kujamiiana tena baada ya kutolewa hospitali wana uwezekano mkubwa wa kufanya tendo hilo mwaka unaofuata.

Nusu ya wanaume na takriban theluthi ya wanawake walizungumza na madakatari wao kuhusu vitendo hivyo vya kujamiiana.

Na chini ya asilimia 40 ya wanaume na asilimia 20 ya wanawake walizungumza na madaktari wao kuhusu kujamiiana katika kipindi cha miezi 12 baada ya kupata maradhi ya moyo.

Mwaka mmoja baadae, zaidi ya theluthi tatu ya wanaume waliripoti kushiriki katika baadhi ya vitendo vya kujamiiana kama ilivyo kwa asilimia 40 ya wanawake.

Lakini asilimia 30 ya wanaume na asilimia 40 ya wanawake wana uwezekano wa kuripoti kutojamiiana sana katika kipindi cha mwaka mmoja, ukilinganisha na kabla ya kupata maradhi ya moyo, kama hawakupewa maelezo ya kurejea kufanya tendo hilo.

' Kiafya'

Dr Lindau amesema: " Idadi kubwa ya wagonjwa wa maradhi ya moyo bado wana uwezo wa kujamiiana. Lakini kwa asilimia kubwa, madakatari wameamua tu kutojadili swala hili na wagonjwa wao baada ya kupata mshtuko wa moyo."

Amesema hata tendo hilo linapojadiliwa, hakuna njia ya kuonyesha kuwa wagonjwa waliambiwa nini, na iwapo taarifa zilikuwa sawa.

Ameongeza kuwa swala la kujamiiana lisipuuzwe kwasababu tu mgonjwa ana umri mkubwa au yumo ndani ya ndoa.

"Huwezi kutabiri kwa kumwangalia mtu kama ana uwezo wa kujamiiana. Wagonjwa hulichukulia tendo hilo kama sehemu muhimu katika maisha yao, na wanahisi madaktari wana wajibu wa kulizungumzia."

Cathy Ross, muuguzi kutoka British Heart Foundation amesem, " Unaweza kufurahia tendo la kujamiiana, hata kama una maradhi ya moyo."

"Na kama ilivyo kwa mazoezi mengine, tendo la kujamiiana linaweza kuleta matatizo kama una maradhi ya moyo kwa hiyo uwe na dawa zako karibu."

"Kupapasana na kuwa karibu na mwenzako ni njia nzuri ya kurejesha uwezo wa kujamiiana na kuongeza kujiamini."