Israel yatakiwa iondoe marufuku ya Gaza

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameitaka Israel kuondoa haraka marufuku ya kuingiza misaada katika Ukanda wa Gaza.

Hii ni kufuatia shambulio lililofanywa na majeshi yake dhidi ya meli zilizokuwa zimechukua shehena ya misaada kuwapelekea Wapalestina katika eneo hilo.

Bwana Ban ameitaja marufuku hiyo kama isiyokuwa na manufaa, isiyo endelevu na mbaya.

Lakini mapema akitetea shambulio hilo, waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alieleza bayana kuwa amri ya kuzuia misafara ya kwenda Gaza itasalia.

Baada ya mkutano wa jumuiya ya nchi za kiarabu nchini Misri, shinikizo zilitolewa kwa umoja wa mataifa kuhakikisha kuwa marufuku hiyo ya Israel imeondolewa. Aidha licha ya kuitishwa uchunguzi wa kina na wa wazi kuhusu mashambulizi hayo, Marekani na Israel zimesema sharti uongozwe na waisraeli wenyewe.