Ivory Coast kupimana na Ureno

Didier Drogba
Image caption Didier Drogba

Mchuano mzito unatazamiwa siku ya Jumanne kati ya Ivory Coast na Ureno katika uwanja wa Nelson Mandela Bay, mjini Port Elizabeth.

Huu utakuwa mchuano wa kundi la G, ambalo pia linajumuisha mabingwa mara tano Brazil na Korea Kaskazini.

Bado haijabainika ikiwa mshambuliaji wa Ivory Coast Didier Drogba ataweza kucheza kutokana na jeraha la mkononi alilopata kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Japan.

Ikiwa Drogba hatacheza, nafasi yake ya ushambuliaji itashikiliwa na Seydou Doumbia wa klabu ya CSKA Moscow, akisaidiana na Salomon Kalou.

Kolou Toure huenda akashikilia nafasi ya nahodha, na ushirikiano na kaka yake Yaya Toure, Didier Zokora na Emmanuel Eboue utaweza kuziba kiasi kikubwa cha pengo lililoachwa na Didier Drogba.

Kocha wa Ivory Coast Sven Goran Eriksson ambaye zamani alikuwa kocha wa England anaielewa vizuri Ureno, iliyoiondoa England katika robo fainali za Kombe la mataifa ya Ulaya mwaka 2004, kupitia mikwaju ya penalti.

Ureno watatumainia kwamba mshambuliaji wao Cristiano Ronaldo ataweza kuendeleza umahiri aloyoonyeshakatika klabu yake ya Real Madrid kufikia mwisho wa msimu.

Lakini changamoto iliyopo ni kwamba Ronaldo alishindwa kuifungia Ureno hata bao moja kwenye michuano 7 ya kufuzu na baadaye akapatwa na jeraha lililomlazimisha kukosa mechi zilizofuatia.

Kocha wa Ureno Carlos Queiroz pia anao wasiwasi kuhusu kiungo Simao Sabrosa kufuatia hali ya kutoridhisha katika klabu yake ya Atletico Madrid na pia kwenye michuano ya kirafiki ya hivi karibuni.

Wasiwasi huo ulizidishwa na jeraha la kiungo aliyetegemewa zaidi Nani, ambaye naye amelazimika kuyaaga mashindano kutokana na jeraha.

Mchuano huo baina ya Ivory Coast na Ureno unao uzito wa kuweza kuashiria nani kutoka kundi hilo la G ambalo pia linajumuisha Brazil na Korea kaskazini ataweza kusonga mbele.