Tuzo ya Mo Ibrahim yakosa mshindi

Mo Ibrahim
Image caption Mo Ibrahim

Tuzo yenye thamani kubwa duniani inayotolewa kwa mtu binafsi, haitotolewa tena kwa mwaka wa pili mfululizo baada ya kuonekana hakuna anayestahili kushinda.

Mfanyabisahara wa Sudan Mo Ibrahim amekuwa akitoa dola za kimarekani milioni tano kwa waliokuwa viongozi wa Afrika kuhamasisha utawala bora katika bara hilo.

Amesema, " Viwango vilivyopangwa kwa mshindi wa zawadi hiyo ni vya juu," akiongeza kuwa hakuna wagombea wapya walioibuka tangu mwaka jana. Washindi lazima wawe wamechaguliwa kwa misingi ya demokrasia na kukubali kuachia madaraka baada ya kukamilisha muda wake.

Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, Olusegun Obasanja wa Nigeria na John Kufuor wa Ghana ni miongoni mwa waliokuwa na sifa ya kupata tuzo hiyo baada ya kuachia ngazi katika miaka mitatu ya awali.

Taarifa kutoka kwa wakfu wa Mo Ibrahim, " Ni wazi kuwa itapita miaka kadhaa bila ya zawadi hiyo kutolewa. Mwaka uliopita, hakuna wagombea wapya walioibuka."

Washindi hupokea dola za kimarekani milioni tano kwa zaidi ya miaka 10, halafu dola 200,000 kwa mwaka mpaka atakapoaga dunia.

Bw Ibrahim anasema zawadi hiyo inahitajika kwasababu viongozi wengi kutoka nchi za bara la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara hutoka katika familia maskini na hivyo hushawishika kung'ang'ania madaraka kwa hofu ya kurudi kwenye umaskini baada ya kung'atuka.

Aliyekuwa Rais wa Botswana Festus Mogae alishinda zawadi hiyo mwaka 2008 baada ya kukaa madarakani kwa mihula miwili katika nchi hiyo yenye matukio machache ya rushwa na yenye maendeleo.

Mshindi wa kwanza kabisa alikuwa Joaquim Chissano, aliyekuwa Rais wa Msumbiji, ambaye tangu wakati huo amekuwa mpatanishi wa migogoro katika nchi mbalimbali za Afrika.