Biashara ya almasi huenda ikazua ghasia

Rais Mugabe akiwa na Mkewe
Image caption Rais Mugabe akiwa na Mkewe

Ripoti mpya imedokeza kuwa maafisa wakuu wa kijeshi na wanasiasa nchini Zimbabwe, wanatumia ghasia kuthibiti bishara ya Almasi.

Ripoti hiyo iliyotolewa na shirika la Global Witness, imesema mamia ya watu wameuawa katika eneo la Murange lenye utajiri mkubwa wa madini ya almasi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Baadhi yao wanasema walipigwa, kubakwa na kulazimishwa kuchimba madini hayo na wanajeshi na polisi wa nchi hiyo.

Ripoti hiyo inadi kuwa kampuni zilizoteuliwa na serikali ya muungano nchini humo, kuimarisha hali ya wachimba migodi yana uhusiano na rais wa nchi hiyo Robert Mugabe, ambaye anazitumia kama vyanzo vya fedha za kufadhili kampeini yake na chama chake cha Zanu PF.

Shirika hilo sasa limependekeza Zimbabwe kuondolewa kama mojawapo ya nchi zinazoshiriki kwenye mazungumzo yanayofanyika mjini Kimberley.

Mazungumzo hayo ya kimataifa yananuiwa kuzuia uuzaji wa almasi inayokisiwa kusababisha mateso na maafa kwa raia.