'Muuaji' Kenya afunguliwa mashtaka

Philip Onyancha
Image caption Philip Onyancha

Muuaji aliyekiri mwenyewe nchini Kenya amefunguliwa shtaka la kumwuua mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka tisa mwezi Aprili.

Philip Onyancha, mwenye umri wa miaka 32, na wanaoshukiwa kushirikiana naye walifikishwa katika mahakama kuu kwenye mji mkuu, Nairobi.

Tangu akamatwe wiki mbili zilizopita, amekuwa akiwaongoza polisi kusaka miili ya anaodai kuwaua.

Amesema ameua watu 19 na alikuwa na nia ya kuua watu 100 baada ya kujiunga na madhehebu yaliyomwambia anywe damu zao ili kupata maisha mazuri.

Amesema mwalimu wake alimwuunganisha katika madhehebu hayo alipokuwa shule, ambaye alikamatwa wiki iliyopita na kuhojiwa na polisi.

Richard Katola, mkuu wa kitengo maalum cha kuzuia uhalifu, amesema mashtaka mengi zaidi ya mauaji yanatarajiwa kutolewa, lakini baadhi ya miili ya watu hao yameshindwa kutambuliwa.

Amesema, " Nyaraka zilizo tayari ni za wale waliouawa na kutambulika au wengine ni baada ya ndugu kutambua vitu vya jamaa zao kwenye eneo kulikofanyika mauaji hayo."

Kulingana na gazeti la Kenya la East African Standard, Bw Onyancha alikamatwa baada ya baba wa mtoto mwenye miaka tisa Anthony Njirua Muiruri aliporipoti kulipa kikombozi kwa watu waliodai kumteka mwanawe.

Polisi walifanikiwa kumpata Bw Onyancha kupitia simu ya mkononi ya Samuel Muiruri aliyotumia kumtumia pesa.

Baada ya kukamatwa, Bw Onyancha alikiri kuhusika na mauaji mengine, wakiwemo makahaba, na kuwapeleka yalipokuwa mabaki ya mwili wa Anthony Muiruri.