Mipango ya kura ya maoni imechelewa-Sudan

Rais wa Sudan Kusini
Image caption Rais wa Sudan Kusini

Wanachama wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamesema, kuna haja ya dharura ya kuhakikisha kuwepo kwa maendeleo katika harakati za maandalizi ya kura ya maoni kuhusu uhuru wa eneo la Sudan Kusini.

Akiongea na baraza hilo, afisa mmoja mwandamizi wa Umoja wa Mataifa, amesema kuna hali ya wasi wasi kuhusu muda mdogo uliosalia kabla ya kufanyika kwa kura hiyo ya maoni Januari mwakani.

Inatarajiwa kuwa raia wengi wa Sudan Kusini, wataunga mkono kura hiyo na Umoja wa Mataifa umesema kazi ya kuchora mipaka ya eneo la Kaskazini na Kusni imeanza pamoja na mpango wa kugawana mapato yanayotokana na uuzaji wa mafuta.

Baraza hilo pia limeelezea wasi wasi wake kuhusu kuongezeka kwa ghasia katika jimbo la Darfur Magharibi mwa nchi hiyo.

Takriban watu 500 waliuawa kwenye mapigano kati ya jeshi la serikali na waasi katika eneo hilo mwezi uliopita.

Maelfu ya watu wengine wametoroka makwao katika miezi ya hivi karibuni kukwepa mapigano hayo.