Walala hoi kufaidika Kombe la Dunia?

Image caption Mashabiki wakionyesha furaha zao siku chache kabla ya Kombe la Dunia

Wakati mipango ya kuandaa Kombe la Dunia nchini Afrika ya kusini ikifanyika raia wengi wa nchi hiyo wakiwemo pia walala hoi, walitarajia kunufaika kutokana na wageni watakaokwenda huko kujionea mashindano hayo.

Miongoni mwao ni Angela Ncube, mchuuzi wa barabarani ambapo ukiritimba mkali wa biashara umedidimiza ndoto za wengi akiwemo Ncube, wamiliki wa nyumba na wafanyabiashara.

Waliofaidi hadi sasa ni FIFA, shirikisho la mpira duniani pamoja na mabwanyenye.

Ncube aliiambia BBC kuwa, sisi walala hoi, hatufaidi lolote. Ncube amesema kuwa alilazimishwa kuhama kutoka karibu na uwanja wa mpira huko Johannesburg alipojaribu kuuza pipi na bidhaa ndogo ndogo kwa mamilioni wanaoingia uwanjani.

Maofisa wa FIFA walitabiri kuwa mashindano haya yatainua uchumi wa Afrika ya Kusini utakaowanufaisha raia wengi na kuimarisha biashara hivyo kuleta ajira kwa wengi.

Taarifa ya shirikisho hilo imesema kuwa haijawakwaza wachuuzi wenye biashara ndogo ila imewapa fursa wenye biashara za wastani waweze kunufaika ili kujenga nafasi za ajira.

Licha ya taarifa ya wakuu wa FIFA, ni vigumu kukubaliana nao ukichunguza hali halisi ya maisha ya wananchi wa kawaida.

Polisi na walinzi wamezingira viwanja vinavyotumiwa kwa mashindano haya, wakichunguza mihadarati inayoweza kusababisha ghasia. Wananyang'anywa chakula au kinywaji kisichotoka kwa makampuni yaliyosajiliwa na FIFA au mamlaka nyingine.

Umasikini wa kupindukia pamoja na ukosefu wa ajira unaokadiriwa kufikia asilimia 25 umesababisha mamia ya watu kumiminika mitaani wakijaribu kuuza bidhaa ili kukidhi maisha. Wengi wao wamekuwa wakiuza bendera, jezi na kofia zinazohusiana na Kombe la Dunia kwa raia wenzao lakini wamezuiliwa kuwasogelea wageni.

Ndani ya viwanja, bidhaa kama pombe ya wadhamini maalum Budweiser inaruhusiwa lakini pombe maarufu nchini humo inayotengenezwa na kiwanda cha pili kwa ukubwa duniani SAB Miller hairuhusiwi.

Hata hivyo kampuni hiyo imefanikiwa kuuza bidhaa zake katika maeneo ya wazi ambako mkono wa FIFA haufiki.

Watalii wachache, upungufu wa fedha

Afrika ya Kusini ilitarajia mamilioni ya watalii lakini ukweli wa mambo ni kwamba imepokea hadi watu 370,000 au chini yake. Wengi wakihofia maisha yao, wakiogopa gharama kubwa na uhalifu.

Wamiliki wa hoteli, migahawa na biashara zinazotegemea utalii imewabidi wapunguze matumaini ya kipato kikubwa walichotarajia.

Waimbaji wa nchi hiyo ambao ni maarufu kote duniani, walitarajia vibarua lakini wasanii kama Black Eyed Peas na Shakira ndiyo waliobahatika kwenye sherehe rasmi. Lakini kundi la wamiliki wa nyumba na mawakala wa biashara ya nyumba waliodhani watapandisha bei za kupanga nyumba wakati wa Kombe la Dunia wamejikuta katika majonzi makubwa na nyota ya jaha imekuwa janga.