Argentina yafuzu raundi ya pili

Image caption Mshambuliaji wa Real Madrid, Gonzalo Higuain aliifungia Argentina

Argentina imekuwa timu ya kwanza kufuzu kwa raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini baada ya kuifunga Korea Kusini mabao 4-1 katika uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg.

Mshambuliaji wa klabu ya Real Madrid Gonzalo Higuain alifunga mabao 3, moja katika kipindi cha kwanza na mawili katika kipindi cha pili.

Kwa sasa Huguain ndiye mchezaji anayeongoza kwa kufunga mabao mengi.

Kwa matokeo hayo Argentina imetuma ujumbe kwamba ni mojawapo ya nchi zinazopania Kombe la Dunia, na ina uwezo wa kulinyakua.

Korea Kusini walijifunga bao la kwanza kupitia Park Chu-Young baada ya kwaju la Lionel Messi kumgonga gotini na kuelekea wavuni.

Muda mfupi kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika Lee Chung-Yong aliifungia Korea Kusini bao la pekee, kufuatia kosa la Martin Dimichelis aliyechelewa kuoondosha mpira kwenye mstari wa goli.